Raia wa Guinea Bissau waandamana

Waziri Mkuu wa Guinea Bissau

Maelfu ya raia wa Ginnea Bissau wameandamana kushinikiza kung'atuka kwa Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior.

Waandamanaji hao wameilalamikia serikali kwa kushindwa kukabiliana na mfumuko wa bei. Aidha raia hao hawajaridhirika na jinsi uchunguzi wa mauaji ya rais Joao Bernardo Viera unavyoendeshwa.

Duru kutoka Guinea Bissau zinasema kwamba Kati ya watu elfu tano na kumi walijitokeza katika barabara kuu ya mji mkuu wa Bissau, katika kile kimetajwa kama maandamano makubwa zaidi kuwahi kufanyika.

Wanachama wa upinzani wamemtaka Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior kuachia madaraka.

Wamemlaumu Waziri Mkuu kwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa rais Joao Bernardo Viera, Mkuu wa jeshi pamoja na wanasiasa wawili miaka miwili iliyopita.

Jopo maalum lililoundwa kuchunguza mauaji hayo halijatoa ripoti yeyote kufikia sasa. Waandamanaji aidha walionyesha ghathabu yao kutokana na mfumuko wa bei. Guinea Bissau ni moja wapo na nchi masikini zaidi duniani.

Raia hao wameapa kuendelea na maandamano hadi pale Waziri Mkuu atakapong'atuka madarakani.

Katika nchi ambayo inakabiliwa na tisho la uthabiti , msukosuko wa kisiasa huenda ukachochea mwingilio wa jeshi ambalo limekuwa na mchango mkubwa wa kisiasa nchini humo hususan endapo jeshi litaamua kuungana na raia wanaoandamana.