Nato kuwasilisha mpango wa amani Libya

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bibi Clinton na Waziri William Hague wa Uingereza, Uturuki

Nchi za Magharibi na wanadiplomasia wa nchi za Kiarabu zinaandaa mpango wa kumaliza mgogoro wa Libya na utawasilishwa kwa Kanali Gaddafi, waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesema.

Akizungumza katika mkutano wa nchi za NATO, Franco Frattini amesema wajumbe wamekubaliana kulitambua Baraza la Taifa la Mpito kama mamlaka halali nchini Libya.

Amesema hilo litamfanya Kanali Gaddafi kutokuwa na ‘njia nyingine’ isipokuwa kuachia madaraka.

Wajumbe wengi katika mkutano huo tayari wamshalitambua baraza hilo la NTC.

Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Alain Juppe, na yule wa Uingereza William Hague ni miongoni mwa wanaoziwakilisha nchi zaidi ya 30 katika mkutano huo mjini Istanbul, Uturuki.

Mkutano wa nne wa kundi hilo tangu mwezi Machi umeitwa kuangalia hatua inayofuata katika kampeni zao Libya.

Bw Frattini amesema Mjumbe wa Umoja wa Matifa nchini Libya Abdul Elah al-Khatib, atawasilisha mapendekezo hayo kwa uongozi na kufanya mazungmzo kwa niaba ya kundi hilo.

"Mpango huu wa kisiasa ni pendekezo linalotaka kumaliza mapigano pia," alisema.

Bw Frattini alisema Bw Khatib atakuwa ndiye afisa pekee atakayeruhusiwa kufanya mazungumzo hayo.

Afisa mwandamizi kutoka Marekani aliyeko kwenye msafara na Bibi Clinton amenukuliwa na Reuters akisema kuwa "nchi zinaanza kuangalia mbali zaidi baada ya Gaddafi,”

"Ataondoka, na mkutano unaweza kuwa mahali pazuri pa kutathmini na kuandaa hatua za mpito.

Mkutano utajadili hatua za kuongeza shinikizo kwa utawala wa Libya kama vile kudhibiti shirika la serikali la Utangazaji. Pia utaangalia ripoti ya Libya juu ya mipango ya wapinzani kuelekea

Wawakilishi wa Baraza la mpito la Benghazi watahudhuria mkutano lakini wamekataa mwaliko wa China na Urusi.

Mgogoro wa Libya unaonekana kuzidi kuendelea. Waasi wanashikilia Mashariki ya Libya na baadhi ya viunga vya magharibi.

Kanali Gaddafi anaendelea kushikilia mji mkuu Tripoli, licha ya kampeni za mashambulio 6,000 ya Nato dhidi ya majeshi ya serikali.

Vikwazo vya kimataifa pia vimewekwa na hati za kuwakamata viongozi waandamizi wa serikali ya Libya zimetolewa

Mjini Tripoli, serikali ya Kanali Gaddafi imekuwa ikiendesha mazungumzo juu ya usambazaji wa mafuta nchini humo.

Baada ya mkutano na na Waziri Mkuu al-Baghdadi al-Mahmoudi alionyesha kumalizika kwa uwekezaji wa Italia wa Euro 30 bilioni (£26 bilioni) na kuwataka wabia wapya kujiunga nao katika kuchimba na kusafisha mafuta

Katika mji huo mkuu, kulikuwa na foleni ndefu zinazofikia zaidi ya maili moja katika vituo vya petrol. Inaripotiwa kuwa bomba muhimu la mafuta katika mji limekatwa na waasi.