Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

RADI YAUA BABA NA MWANA

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Radi haipigi sehemu moja mara mbili?

Bwana mmoja nchini Marekani amekufa baada ya kupigwa na radi, ikiwa ni miaka 48 baada ya baba yake naye kufa kwa kupigwa na radi.

Bwana huyo Stephen Rooney alikufa mwishoni mwa wiki wakati akiwa mapumzikoni na familia yake. Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa NBC muda mfupi kabla ya kupigwa na radi hiyo, bwana Rooney alisema kimzaha kuwa "Msiwe na wasiwasi, radi haipigi sehemu moja mara mbili" Akimaanisha kuwa kwa kuwa baba yake alipigwa na radi, si rahisi na yeye kupatwa na mkasa huo.

Baba yake Rooney alipigwa na radi wakati akivua samaki katika eneo la Fortscue, New Jersey, wakati Stephen akiwa na miaka mitano.

NBC imeripoti kuwa bwana Stephen alikuwa na binamu yake, wakati alipopigwa na radi hiyo. Watu hao waliokuwa wakijikinga na manyunyu walikuwa wakivuta sigara karibu na mti wakati radi ilipoanguka, wamesema polisi.

ASALI BARABARANI

Usafishaji ndio kwanza umemalizika, wa kusafisha asali iliyomwagika na takriban nyuki milioni kumi na nne waliozagaa, baada ya gari lililokuwa limewabeba kupinduka nchini Marekani.

Image caption Nyuki kila mahali...

Mamlaka za usalama za Freemont zimesema polisi kadhaa walingatwa na nyuki hao wakati wa kufanya shughuli ya kuwakamata. Mamlaka zinasema gari lililokuwa likiwasafirisha nyuki hao pamoja na asali kutoka California kwenda North Dakota lilipoteza mwelekeo na kupinduka huku likiwa na mizinga mia nne ya nyuki na asali.

Watu walioshuhudia waliona wingu kubwa jeusi likielekea hewani, na taarifa kusema walikuwa ni nyuki wakiingia mitini.

Mamlaka zilifanya kazi siku nzima kuondoa asali barabarani, ingawa bado kulikuwa na nyuki kadhaa wakiendelea kurandaranda hewani.

KACHINJA PANYA

Image caption Panya

Mwanamama mmoja nchini Australia amekiri makosa ya utesaji wanyama, baada ya kujipiga picha ya video ikionesha akichinja panya.

Msichana huyo Naomi Anderson alijipiga picha akimkata kicha panya na kuweka video hiyo kwenye mtandao, katika ukurasa wa facebook.

Mahakama moja mjini Brisbane ilimpa msichana huyo hukumu ya kufanya kazi za jamii kwa saa mia moja na themanini kama adhabu ya kosa hilo alilofanya mapema mwezi huu.

Mahakama iliambiwa kuwa msichana huyo alitumia kisu cha kukatia nyama kumchinja panya huyo.

Gazeti la Times of India limesema panya huyo alikufa sekunde arobaini baada ya kuchinjwa. Bi Naomi aliziweza picha za video kwenye mtandao akitumia jina la uongo, ingawa baadaye alikamatwa. Kwa mujibu wa sheria za wanyama za Queensland, msichana huyo angeweza kupata adhabu ya kifungo cha miaka mwili jela.

MZUNGU KAGEUKA MGANGA WA KIENYEJI

Haki miliki ya picha Reuters (audio)
Image caption Mganga

Bwana mmoja aliyekuwa akifanya kazi benki hapa Uingereza, ameamua kuacha kazi hiyo na kuwa mganga wa kienyeji Afrika Kusini.

Bwana huyo Thomas Heathfield alipatiwa mafunzo ya kuwa mganga wa kienyeji, ikiwa ni pamoja na kukaa siku tatu bila kulala, na kucheza usiku, kila siku pamoja na kunywa damu ya mbuzi.

Bwana huyo pia alipitia mitihani mbalimbali, ambayo hyaijatajwa, ili kuthibitisha kuwa anafaa kuwa sangoma.

Heathfield alipatiwa jina la Gogo Mndawe baada ya kuweza kujifunza kuzungumza ki- sisiswati na pia kufaulu mitihani kwa miezi mitatu katika kijiji kimoja kilichopo katika jimbo la Mpumalanga, Afrika Kusini.

"Baba yangu na mama yangu walikuja siku nilipomaliza mafunzo, pamoja na wanakijiji kama mia mbili hivi" amesema bwana Heathfield akikaririwa na gazeti la The Sun.

Bwana huyo amesema alipata mwamko wa kiroho, uliomfanya aache kazi yake yenye kipato kikubwa.

SHEREHE ZA KUACHANA

Sherehe za kusherekea kupeana talaka zimeendelea kupata umaarufu nchini Japan, baada ya tetemeko la ardhi, tsunami na janga la kinuclear kusababisha wanandoa kutazama upya maisha yao.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wakivunja pete..

Sherehe moja ya kupeana talaka hugharimu takriban yen elfu hamsini na tano, sawa na takriban dola mia nane. Sherehe hizo hujumuisha kupika chakula na pia kuvunja pete za harusi kwa kutumia nyundo.

Tomoharu Saito ambaye alifanya sherehe ya kumtaliki mkewe Miki amesema alihisi shughuli ya kuvunja pete ikimsafisha. "Pete zilikuwa ngumu kuvunja, lakini hatimaye tulifanikiwa" amesema Saito.

Sherehe hiyo pia hujumuisha kuvaa gauni la talaka, na Miki alivaa gauni la manjano. Shirika la habari la Reuters limesema Hiroki Terai ambaye ndio huandaa sherehe za talaka nchini Japan, na ambaye aliandaa sherehe ya kwanza miaka miwili iliyopita amesema mpaka sasa amekwisha andaa sherehe themanini za ndoa kuvunjika.

Naam bila shaka, kule kwetu tunavyopenda sherehe za harusi--- Kitchen Party, bachelor party, hen party, send off party, reception party, harusi yenyewe--- na sasa tumepata sababu nyingine tena… Dovorce party.. kazi kwenyu.

Na kwa taarifa yako….

Takriban watoto mia mbili huzaliwa duniani kila dakika moja.

Tukutane wiki ijayo… Panapo majaaliwa..