Mashtaka yapunguzwa kwa washukiwa

Washukiwa Zimbabwe Haki miliki ya picha ap
Image caption Washukiwa Zimbabwe

Mashtaka yamepunguzwa dhidi ya wanaharakati sita wa Zimbabwe walioshutumiwa kwa uchochezi baada ya kuhudhuria mhadhara mwezi February kuhusu mapinduzi ya Misri.

Kwa sasa wanashtakiwa kwa kuchochea ghasia kwa umma na kwa hiyo wanakabiliwa na kifungo cha miaka 10 badala ya kifo kama ilivyonuiwa wakati kesi hiyo ilipoanza mwezi Agosti.

Warsha iliandaliwa na mhadhiri mmoja wa chuo kikuu kwa kichwa "Ni somo gani tunaweza kujifunza"- kichwa ambacho upande wa mashtaka ulisema kina maana ya kupanga njama za kuiga yaliofanywa Misri.

Wote wamekanusha mashtaka hayo. Mashtaka sawa na hayo dhidi ya wanaharakati wengine 40 yamefutiliwa mbali.

Mhadhiri wa somo la sheria katika Chuo kikuu cha Zimbabwe Munyaradzi Gwisai, ambaye wakati mmoja alikuwa mbunge wa chama cha MDC ni miongoni mwa walioshtakiwa ambaye kesi yake imesogezwa hadi tarehe 22 mwezi Augosti.

Katika warsha yake iliyofanyika February 19, video kuhusu maandamano ya Misri iliyoneshwa kwa washiriki.

Wanaharakati hao sita wanahusishwa na shirika la kimataifa la kisosholisti- kundi ambalo huwatetea watu masikini na kuwepo na usawa katika ugawaji rasilimali.

Washutumiwa hao wanasema kuwa mkutano wao ulinuiwa kujadili masuala muhimu kuwahusu watu wa kipato cha kati wa Zimbabwe na kuwa wanajifunza nini kutokana na matukio ya kaskazni mwa Afrika.

Miaka miwili iliyopita chama cha Rais Robert Mugabe cha Zanu-PF na kile cha MDC cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai viliunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ilionuiwa kuinua uchumi na kuleta mabadiliko katika mfumo mzima wa uchaguzi nchini Zimbabwe.

Mwezi April, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye ni mpatanishi wa mzozo wa Zimbabwe alimuonya Rais Mugabe akisema kuwa matukio ya kaskazini mwa Afrika hayapaswi kupuuzwa na kwamba Mugabe alitakiwa kuweka mambo sawa nchini mwake. Bw Zuma amesema kuwa masuala kuhusu haki za binadamu yanapaswa yashughulikiwe miongoni mwa masuala mengine mengi .