Aston Villa yamsajili Shay Given

Klabu ya Aston Villa imekamilisha usajili wa mlinda mlango wa Kimataifa wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland akitokea klabu ya Manchester City.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Shay Given

Given mwenye umri wa miaka 35 amesaini mkataba wa miaka mitano hapo Villa Park baada ya vilabu hivyo viwili kukubalina ada ambayo haijatajwa ni kiasi gani.

Meneja mpya wa Villa Alex McLeish alikuwa amemlenga Given baada ya mlinda mlango wao wa kutumainiwa Brad Friedel kujiunga na Tottenham.

Given ameeleza katika mtandao wa klabu hiyo: "Aston Villa ni klabu kubwa na nimefurahi sana kujiunga nayo. Ni changamoto mpya na nimepania kuikabili."

Mlinda mlango huyo alikuwa hapangwi baada ya meneja wa Manchester City kuamua mlinda mlango wa timu ya taifa ya England Joe Hart kuwa changuo lake la kwanza.

Given atacheza mechi yake ya kwanza akiwa na Villa siku ya Alhamisi watakapopambana na Walsall.

Ni mchezaji wa kwanza kusajiliwa na McLeish tangu alipochukua hatamu ya kuinoa Aston Villa na meneja huyo wa zamani wa Birmingham anaamini Given atakuwa na mchango mkubwa katika klabu hiyo.