Corinthians wajitoa kumsajili Tevez

Mchakato wa Carlos Tevez kuihama Manchester City na kuelekea klabu ya Corinthians umesshindwa kutekelezwa kwa sababu timu hiyo ya Brazil imejitoa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Carlos Tevez

Manchester City ilikuwa ikifikiria ada ya paundi milioni 40 imekubaliwa kwa mshambuliaji huyo wa Argentina baada ya kuiambia Manchester City anataka kuihama na kuelekea Amerika Kusini.

Lakini klabu ya Corinthians imesema hakuna muda wa kutosha kuweza kumsajili Tevez mwenye umri wa miaka 27 kabla ya dirisha la usajili halijafungwa saa kumi jioni siku ya Alhamisi.

Corinthians bado wanamuhitaji Tevez na wamedokeza makubaliano yataweza kufikiwa mwezi wa Januari.

Ilionekana mshambuliaji huyo wa zamani wa West Ham amepata kile alichokuwa akihitaji, ambacho ni uhamisho, lakini baadae katika taarifa yao klabu ya Corinthians imesema: "Bodi ya klabu ya Corinthians inatangaza rasmi kuondoa uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Argentina Carlos Tevez.

"Wakati wakipongeza jitahada za Manchester City kwa kuhusika na mazungumzo yote, muda zaidi unahitajika kwa ajili ya kufanikisha uhamisho, hasa ikizingatiwa usajili wa wachezaji kutoka nje unafungwa siku ya Jumatano tarehe 20 mwezi wa Julai kwa saa za Brazil.