Siasia amuita Odemwingie timu ya taifa

Mshambuliaji wa Nigeria Peter Osaze Odemwingie amerejeshwa katika kikosi cha timu ya taifa baada ya kumaliza tofauti zake na kocha Samson Siasia.

Image caption Osaze Odemwingie

Odemwingie aliondolewa katika timu ya taifa mwezi wa Machi baada ya kuondoka katika kambi ya mazoezi bila ruhusa, na kukosa mechi ambayo Super Eagles iliishinda Argentina kwa mabao 4-1 na pia mechi waliyotoka sare ya 2-2 dhidi ya Ethiopia, katika mchezo wa kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Mshambuliaji huyo anayechezea klabu ya West Bromwich Albion amejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 22 cha Nigeria kwa mechi ya kirafiki mwezi wa Agosti dhidi ya Ghana itakayochezwa mjini London.

Hivi karibuni Shirikisho la Soka la Nigeria lilisema Odemwingie na Siasia wamemaliza tofauti zao na mchezaji huyo amejirudi.

Siasia, ambaye awali aliapa kutomruhusu Odemwingie kurejea katika timu ya taifa hadi atakapoomba radhi, amethibitisha tatizo limesuluhishwa.

"Kwa sasa tupo pamoja na mambo yanaweza kusonga mbele kwa manufaa ya soka ya Nigeria," alisema Siasia.

Pia katika kikosi hicho yumo mshambuliaji wa timu ya Fenerbahce, Emmanuel Emenike ambaye alikamatwa mwezi huu nchini Uturuki akihusishwa na uchunguzi wa kupanga matokeo.

Aliachiwa baadae bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

Nigeria itatumia mechi hiyo ya kirafiki dhidi ya Ghana kujiandaa kwa mchezo wake dhidi ya Madagascar wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwezi wa Septemba.

Mabingwa hao mara mbili wa Afrika wapo nyuma ya Guinea vinara wa kundi B kwa pointi tatu katika kutafuta nafasi ya kufuzu moja kwa moja mashindano yatakayofanyika Gabon na Equatorial Guinea.