Rais wa Malawi asema yuko tayari kuzungumza

Rais Bingu wa Mutharika
Image caption Rais Bingu wa Mutharika

Maafisa wa matitabu kutoka hospitali moja nchini Malawi wanasema kuwa kwa uchache watu 18 wameuawa katika ghasia za maandamano nchini humo.

Jeshi limepelekwa katika mji mkuu wa Lilongwe, wakati huu ambapo maandamano yamerejelewa katika miji jirani.Msemaji wa polisi amethibitisha kifo kimoja tu lakini maafisa kutoka hospitali wanasema watu wanane wameuawa.

Waandamanaji wameghadhabika na kuongezwa kwa bei za bidhaa na vile vile na Rais Bingu wa Mutharika.

Rais wa Mutharika amelihutubia taifa na kusema yuko tayari kwa mazungumzo na wapinzani na makundi ya kiraia. Makundi ya kiraia yalioandaa maandamano hayo yanasema kuwa Malawi inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi tangu uhuru kupatikane miaka 47 iliyopita.

Serikali hivi karibuni iliidhinisha bajeti ya kubana matumizi na kuongeze kodi ili kupunguza kutegemea misaada baada ya wafadhili wengi kukatiza misaada yao kwa Malawi.

Wafadhili wameishutumu Malawi kwa kufuja uchumi na kukosa kuzingatia haki za binadamu.

Maandamano haya yamefanyika katika miji mingi lakini vifo vimetokea katika mji wa Mzuzu kilomita 300 Kaskazini mwa Lilongwe.

Askofu Maurice Munthali naibu katibu mkuu wa kanisa la Kipresbyteri aliyekwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti kutambua waliouawa amesema wote waliokufa wanaonesha walipigwa risasi, jambo ambalo limethibitishwa na wauguzi.

Askofu huyo amesema pia baadhi ya wale walio hospitali hawakushiriki katika maandamano bali walijikuta katikati ya vurugu hizo.

Taarifa zaidi zasema kuwa mali ya Waziri mmoja wa serikali imeshambuliwa na waandamanaji katika mji huo.

Baadhi ya waandamanaji hao wanamtaka Rais Bingu wa Mutharika ajiuzulu.Polisi nao wametumia gesi za kutoa machozi mjini Lilongwe kuwatawanya waandamanaji na vile vile wameweka vizuwizi kuwazuia watu kuingia katika mji huo.

Mmiliki wa radio moja ya kibinafsi nchini humo Alaudin Osman ameiambia BBC kuwa ameagizwa na vyombo vya utawala kutopeperusha matangazo ya moja kwa moja kwa kuwa inadaiwa yanachochoea kinachoendelea hivi sasa.

Malawi ni moja wapo ya nchi masikini zaidi ulimwenguni ambapo asili mia 75 ya idadi ya watu nchini humo hutumia chini ya dola moja katika matumizi yao ya kila siku.