al-Shabaab: 'Bado haturuhusu mashirika ya misaada ya Magharibi'

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wananchi wa Somalia wakihitaji msaada

Kundi la al-Shabaab limekanusha kuondoa amri yake ya kuzuia mashirika ya misaada ya Magharibi na kupinga kuwepo kwa njaa Somalia

Kundi hilo limekanusha kuwa limeondoa amri yake ya mwaka 2009 ya kupiga marufuku mashirika ya misaada ya Magharibi na kusema taarifa za Umoja wa Mataifa kuhusu baa la njaa ni ‘propaganda tupu.’

Kadhalika kundi hilo linasema hakuna baa la njaa Kusini mwa Somalia.

Siku ya Jumatano Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kuwa baadhi ya maeneo ya Somalia yanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa muda mrefu katika kipindi cha miaka 60.

Msemaji wa kundi la al-Shabab, lililo na uhusiano na al-Qaeda na linalodhibiti sehemu kubwa ya nchi, limeshutumu vikundi vya misaada kwa kufanya mambo kisiasa zaidi.

Lakini Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa njaa ipo na itaendelea na jitihada zake za misaada.

Mashirika mengi ya misaada ya Magharibi yaliondoka Somalia mwaka 2009 kufuatia vitisho vya al-Shabaab..

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)ni miongoni mwa yale yaliyopigwa marufuku.

Linasema linapanga kutoa misaada hiyo kwa kutumia ndege zinazodondosha chakula ktkka mji mkuu Mogadishu katika siku zijazo kusaidia maelfu ya watoto ambao wanakabiliwa na utapiamlo uliotokana ukosefu wa chakula nchini humo.

Watu milioni 10 inaripotiwa kuwa wanahitaji chakula cha msaada katika Pembe ya Afrika lakini Somalia ndio nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi, hasa kutokana na kutokuwa na serikali ya kitaifa kuratibu misaada baada ya miongo miwili ya mapigano.

Maelfu ya watu wanayakimbia maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabaab na kwenda kwanye kambi zilizoko maeneo yanayodhibitiwa na serikali dhaifu ya mpito inayopigana na wapiganaji wa kiislam.

"Tuna uhakika kabisa kuwa kuna baa la njaa katika maeneo mawili Kusini mwa Somalia," David Orr, msemaji wa WFP Afrika ameiambia BBC.

"Tumeona ushahidi kwenye udharura wa sura na miguu ya watoto alio na utapiamlo ambao walilazimika kukimbia eneo lenye njaa na wakati mwingine kwa siku kadhaa na wiki kadhaa."

Msemaji wa WFP Emilia Casella alisema shirika lake litaendela kufanya kazi mahali panapowezekana kufanya hivyo.

"Al-Shabab sio kundi kubwa. Ni muhimu kujua kwamba tunafanya kazi mahali inapowezekana, tunafanya mpango kufanya kazi mahali ambapo panawezekana," ameliambia Shirika la Habari la AFP.

Wilaya mbili ambazo zina baa la njaa limetangazwa ni –Bakool na Lower Shabelle ziko chini ya udhibiti wa al-Shabab na mashirika ya misaada yamekuwa makini kurejesha shughuli zake huko kutokana na hofu ya usalama wa wafanyakazi wao.

Msemaji wa Al-Shabab Ali Mohamud Rage mapema mwezi huu alitangaza kuwa mashirika ya misaada, yawe ya Kiislam au la yataruhusiwa kurejea nchini Somalia almradi hayana ‘agenda ya siri.’

Hilo limeishawishi Marekani kusema itatondoa marufuku yake na kuruhusu misaada ya chakula katika maeneo yayodhibitiwa na al-Shabab, kundi ambalo Marekani inaliita ni la kigaidi.

Hata hivyo Bw Rage amewaambia waandishi wa habari mjini Mogadishu Alhamisi usiku kuwa: "Mashirika ya misaada yaliyozuiwa bado yamezuiliwa. Mashirika hayo yalikuwa yakijihusha na shughuli za kisiasa."

Anakiri kuwa kuna ukame lakini akasema taarifa kwamba kuna baa la njaa zilikuwa "ni upuuzi mtupu, hazina mashiko kwa 100% na ni propaganda tupu".

"Kuna ukame Somalia na upungufu wa mvua lakini si hali mbaya kama wanavyoileza wao."

Bw Orr alisema hali imefanywa kuwa mbaya kwa sababu ya kuzuiliwa kwa misaada kuwafikia watu wengi.

"Tunaomba wafanyakazi wa misaada waweze kutoa misaada ya kibinadamu. Watu wanasema wana njaa mpaka wanakufa huko. Hii ni hali ya kufa na kupona," aliiambia BBC.

"Hatungekuwa katika hali hii kama misaada ya kibinadamu ingekuwa inafikia jamii. Tunaziomba pande zote zenye kuguswa na hali hii kuturuhusu kwenda huko ili tupeleke misaada haraka na kwa namna inayowezekana."

Rashid Abdi, mchambuzi wa Somalia katika Taasisi ya Kimataifa kuhusu Migogoro ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa al-Shabab walikuwa wanajaribu kuepuka ‘kuonekana kuwa ni watu waliosababisha hali mbaya ya janga la kibinadamu.’

Zaidi ya Wasomali 166,000 wanakadiriwa kuikimbia nchi yao na kuingia nchi jirani za Kenya au Ethiopia katika miezi ya karibuni.

Siku ya Jumatano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema $300 milioni (£184milioni) zinahitajika katika kipindi cha miezi miwili kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na njaa.

"Watoto na watu wazima wanakufa katika hali ya kutisha," alisema.

Karibu nusu ya idadi ya watu wa Somalia milioni 3.7 walikuwa kwenye ukosefu mkali , alisema, wengi wao wakiwa Kusini.

Maeneo haya kwa sehemu kubwa yanadhibitiwa na al-Shabab.