Mshtaki wa Dominique Strauss-Kahn azungumza

Haki miliki ya picha AP
Image caption Nafissatou Diallo katika mahojiano na ABC

Mhudumu wa Hotel mjini New York ambaye anamtuhumu mkuu wa zamani wa IMF Dominique Strauss-Kahn kujaribu kumbaka katika chumba cha hotel amejieleza katika mahojiano kwa mara ya kwanza.

Nafissatou Diallo ameliambia jarida la Newsweek kuwa alisema ukweli kuhusu tukio hilo Mei 14.

Hatua hiyo imekuja wakati mamlaka zinaangalia iwapo mashtaka dhidi ya Strauss-Khan yatupiliwe mbali huku kukiwa na wasiwasi kuhusu ukweli wa madai hayo.

Mwanasiasa huyo wa Kifaransa mwenye umri wa miaka 62, aliyejiuzulu wadhifa wake ua ukuu wa IMF kujitetea dhidi ya madai hayo, amekana mashtaka yote.

Alisema kilichotokea kati yake na Bi Diallo yalikuwa ni makubaliano, na wanasheria wake wameelezea mahojiano ya mhudumu huyo kuwa ‘hayana msingi wowote.’

Bi Diallo ameliambia jarida la ‘Newsweek’: "Nataka afungwe gerezani.Nataka ajue kuna maeneo mengine huwezi kutumia nguvu zako wala pesa yako."

Mhamiaji huyo mwenye umri wa miaka 32 kutoka Guinea ameliambia jarida hilo kuwa aliogopa kupotza kazi yake wakati alipokimbia kutoka chumbani mahali ambapo tukio hilo linadaiwa kutokea.

Lakini wanaomuwakilisha Bw Strauss-Kahn wanamtuhumu mshtaki huyo kwa kuendesha ‘kampeni ya vyombo vya habari’ kuwashawishi waendesha mashtaka kuendelea na kesi dhidi ya mkuu huyo wa IMF, shirika la habari la Reuters limeripoti.

Anashtakiwa kwa makosa saba huku manne kati ya hayo yakiwa ni makubwa, mawili yakiwa ni uhalifu unaohusu vitendo vya ngono, moja la kujaribu kubaka na lingine la unyanyasaji wa kijinsia pamoja na makosa mengine likiwemo la kufngwa kinyume cha sheria.

Lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vinasema kesi hiyo inaelekea kushindwa. Waendesha mashtaka wamesema mhudumu huyo ametoa ushahidi wa uongo kwa majaji, ukionyesha maelezo yanayopishana katika mtiririko wa matukio siku hiyo.

Bw Strauss-Kahn aliachiliwa kutoka kwenye kifungo cha nyumbani Julai Mosi kwa dhamana ya ya fedha $6milioni (£3.7milioni)na mali.

Wakati huohuo, Utawala wa Ufaransa unachunguza tuhuma kuwa Bw Strauss-Kahn alijaribu kumbaka mwandishi wa Ufaransa Tristane Banon muongo mmoja uliopita.

Bw Strauss-Kahn anakanusha kuhusika na makosa hayo, na tayari amefungua kesi ya kupinga madai hayo, akimshtaki Bi Banon kwa taarifa za uongo.

Mpaka alipojitokeza kwa ajili ya mahojiano, jina lake halikuwa kuripotiwa katika vyombo vya habari ambavyo kwa kawaida huhifadhi utambulisho wa watu wanaojitokeza kusema wamenyanyaswa kijinsia.