Goodluck:Muhula mmoja kwa rais

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Goodluck Jonathan

Kiongozi wa Nigeria Goodluck Jonathan amesema kuwa ataomba wabunge kubadilisha katiba ili marais wahudumu muhula mmoja lakini wa muda mrefu.

Katiba ya sasa inaruhusu rais kuhudumu kwa mihula miwili ya miaka minne kwa muhula.

Kumekuwa na taarifa katika magazeti ya nchini Nigeria kwamba mapendekezo ya kubadili katiba ni kwa lengo la kumuongezea muda Rais Jonathan.

Lakini rais,ambaye ndiyo anahudumu muhula wake wa kwanza wa miaka minne, anasema sheria hio haitotumika hadi atakapoondoka madarakani.

" Kama pendekezo la kubadilisha litaidhinishwa na bunge , rais amewahakikishia raia kwamba yeye hatofaidika na mpango huo," shirika la habari la AFP limenukuu taarifa kutoka kwa ofisi ya Bwana Jonathan.

Bwana Jonathan hakusema wazi muhula huo utakuwa wa miaka mingapi, lakini akasema kuwa mabadiliko hayo yataangazia zaidi utawala bora na kuacha suala la kufikiria kuchaguliwa tena.

Mwandishi wa BBC mjini Lagos Jonah Fisher anasema kuwa muhula huo umetajwa kuwa miaka sita.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Ramani ya Nigeria

Taarifa hiyo inasema Bwana Jonathan "ana wasiwasi kuhusu malumbano yanayoletwa na suala la kuchaguliwa tena kwa viongozi baada ya miaka minne".

Takriban watu 500 waliuawa, maelfu ya watu kulazimishwa kuhama makwao na baadhi ya miskiti na makanisa kuchomwa moto baada ya matokeo ya uchaguzi mwezi Aprili kutangazwa.