Abou Diaby kutocheza soka wiki kumi

Kiungo wa Arsenal Abou Diaby atakosa mechi za mwanzo za msimu huu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu.

Image caption Abou Diabu

Diaby, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa akisumbuliwa na kuumia mara kwa mara tangu mwishoni mwa msimu uliopita na hakuwepo katika ziara ya timu ya Arsenal ilipokwenda bara Asia na kambi ya mazoezi nchini Ujerumani.

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger anataraji Diaby kukosa mechi dhidi ya Newcastle, Liverpool na Manchester United.

"Kwa kawaida anatakiwa awe amerejea uwanjani katika ya wiki nane hadi kumi baada ya upasuaji, hii maana yake itakuwa mwishoni mwa mwezi wa Agosti," alisema Wenger.

Arsenal itasafiri hadi Newcastle kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Soka ya England tarehe 13 mwezi wa Agosti, kabla ya kuikaribisha Liverpool katika uwanja wa Emirates tarehe 20 Agosti na tarehe 28 mwezi huo huo, watakaposhuka katika uwanja wa Old Trafford.