Boko Haram kuzungumza na serikali Nigeria

Ramani ya Nigeria
Image caption Ramani ya Nigeria

Serikali ya Nigeria imetangaza kwamba inataraji kufanya mazungumzo na kikundi cha waislamu wenye siasa kali, cha Boko Haram.

Kamati imeteuliwa kuchunguza mtafaruku katika eneo la kaskazini-mashariki mwa nchi, baada ya watu kadha kuuwawa katika mapambano ya karibuni baina ya Boko Haram na jeshi.

Kamati hiyo ya wajumbe 10 imepewa kama wiki mbili kutoa mapendekezo.

Kamati imeagizwa kutazama swala la usalama katika eneo la ghasia la kaskazini-mashariki, na kuanza mazungumzo na kikundi cha Boko Haram, cha Waislamu wa msimamo mkali.

Hivi karibuni wapiganaji wa kikundi hicho, wamefanya mashambulio kadha, hasa dhidi ya askari wa usalama.

Wanajeshi wamezidishwa huko, na wengine wamelipiza kisasi, na wakati mwengine kuuwa raia.

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, anapenda kusema kuwa sera yake ni kuuma na kupuliza.

Lakini hadi sasa kuuma sana kumezidi kuharibu mambo; huku maelfu wamelihama eneo.

Mfano ambao rais anataka kujaribu tena ni ule uliotumiwa katika eneo la Niger Delta; ambako baada msamaha wa serikali, pamoja na fidia kubwa kwa wapiganaji, eneo hilo sasa ni shuwari.

Hadi sasa, Boko Haram hawakuonesha ishara kuwa wanataka kuzungumza.

Siku za nyuma walishikilia kuwa jeshi lazima liondoke kwanza, kabla ya mazungumzo kuanza.