Wahamiaji wa Libya wafa

Haki miliki ya picha Mauro SeminaraAFPGetty Images
Image caption Wakimbizi wa Libya

Walinzi wa pwani huko Italia wamekuta miili ya watu 25 katika boti iliyokuwa imejaa wakimbizi wanaokimbia kutoka Libya.

Boti hiyo yenye mita 15 ilifunga gati katika kisiwa cha Lampedusa kusini mwa Italia iliyokuwa imebeba watu 271 waliookoka, shirika la habari la AFP liliripoti.

Miili ya watu hao 25 ilikutwa kwenye chumba chenye injini ya boti.

Maafisa walisema watu hao wameonekana kufariki dunia kutokana na kukosa hewa ya kutosha.

Maelfu ya wakimbizi kutoka Afrika magharibi wamewasili kwenye kisiwa hicho katika wiki za hivi karibuni.

Walinzi hao wa pwani waliingia katika boti hiyo siku ya Jumatatu na kugundua miili ya watu hao.

Vyombo vya habari vya Italia vimeripoti kuwa watu waliokuwa katika chumba hicho chenye injini walijaribu kutoka lakini walikwama kutokana na idadi ya watu waliokuwemo na huenda wakawa wamekabwa na harufu kali ya moshi kutoka kwenye injini.