Video 'ikionyesha mateka Nigeria'

Image caption Ramani Nigeria

Video moja imetolewa inayodaiwa kumwonyesha raia wa Uingereza na mwenzake kutoka Italia waliotekwa mwezi Mei kwenye jimbo la Kebbi lililopo kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Katika video hiyo, iliyotumwa kwenye shirika la habari la AFP nchini Ivory Coast, ilisema watekaji nyara hao ni kutoka kundi la al-Qaeda.

Inaonyesha mateka hao wakiwa wamezibwa macho na kupiga magoti, huku watu watatu wakiwa wamekamata silaha na kusimama nyuma yao.

Ofisi ya wizara ya mambo ya nje ya Uingereza ilisema ilikuwa ikichunguza kama video hiyo ni ya kweli na kusihi kusiwe na dhana.

Taarifa hiyo ilisema, " Tunajuta kutolewa kwa video kama hii kwa umma na tunasihi vyombo vya habari kuacha kutoa taarifa zisizothibitishwa wakati kama huu wenye utata."

Wizara ya mambo ya nje ya Italia imesihi video hiyo izuiwe na kusema ilikuwa ikifanya kazi kwa karibu na wenzake wa Uingereza na Nigeria.

Ikiwa itathibitishwa, itakuwa mara ya kwanza kwa kundi la al-Qaeda kwa upande wa Afrika kaskazini kufanya shughuli zake Nigeria, nchi maarufu barani Afrika na moja ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani.

Al-Qaeda inafanya shughuli zake zaidi katika eneo la jangwa la Sahara kaskazini mwa Nigeria, Niger, Mali na Algeria.

Wawili hao walikamatwa na watu wenye silaha jioni ya Mei 12 katika hoteli huko Birnin Kebbi, mji mkuu wa jimbo la Kebbi lililo mpakani na Niger.