Tevez aongezewa likizo kurudi Man City

Manchester City imeongeza muda wa likizo ya Carlos Tevez na wanatazamia atarejea mazoezini siku ya Jumatatu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Carlos Tevez

Hii ina maana Tevez atakosa kucheza mechi ya siku ya Jumapili ya kuwania Ngao ya Jumuia dhidi ya Manchester United kwenye uwanja wa Wembley.

Manchester City mapema ilisema awali ilikuwa arejee mazoezini siku ya Alhamisi, ingawa BBC inafahamu kwamba, hadi siku ya Jumatano mchana, Tevez bado alikuwa nje.

Mwezi wa Juni, mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina alisema kamwe hatarejea Manchester "hata kama kwa likizo".

Baadae akaomba kuihama klabu hiyo kwa sababu binafsi, lakini uhamisho wake wa paundi milioni 40 kwenda klabu ya Brazil ya Corinthians ukakwama.

Msemaji wa Manchester City amesema kutakuwa na mazoezi mepesi kwa wachezaji wote wa kikosi hicho siku ya Jumatatu.

"Carlos kwa sasa ameongezewa muda wa likizo yake, kwa hiyo anaweza kurejea siku ya Jumatatu, ambayo itakuwa siku ya 21 tangu Argentina ilipotolewa katika Kombe la Copa America," alisema msemaji huyo wa Manchester City.

Pamoja na Corinthians, mshambuliaji huyo wa Argentina, Tevez amehusishwa pia kujiunga na na klabu za Inter Milan na Real Madrid.