Chelsea yakubali kumsajili Romelu Lukaku

Chelsea imeafiki makubaliano ya kumsajili mshambuliaji kijana kutoka klabu ya Anderlecht Romelu Lukaku.

Image caption Romelu Lukaku

Lukaku mwenye umri wa miaka 18 atajiunga na klabu hiyo ya Chelsea inayojinoa kwa Ligi Kuu ya England, ikisubiria majibu ya afya yake na makubaliano ya mahitaji yake binafsi.

Klabu ya Anderlecht ilitangaza kumuu za Lukaku kupitia mtandao wao, lakini haikubainisha kiwango cha ada. Chelsea inaarifiwa mwezi dau lao la paundi milioni 18 lilikataliwa na klabu ta Anderlecht.

"Ni mchezaji kijana mwenye mtazamo wa mbali," alisema meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas baada ya klabu ya Chelsea kushinda mechi yake dhidi ya Rangers siku ya Jumamosi.

"Kilichobakia hivi sasa ni kujitayarisha labda kumpata mchezaji huyu mwenye kipaji cha kupachika mabao."

Lukaku ni mchezaji maarufu nchini Ubelgiji msimu wa 2009/2010 alipkuwa na umri wa miaka 16 alikuwa mfungaji bora wa ligi ya nchi hiyo.

Wakati Chelsea wakikamilisha taratibu za kumnasa Lukaku, winga wao Yury Zhirkov, ameondoka katika klabu hiyo na kujiunga na klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi.

Image caption Yuri Zhirkov

Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusiana na uhamisho wa Zhirkov lakini taarifa kutoka Urusi zimesema uhamisho wake utakuwa wa paundi milioni 13.2.

Zhirkov mwenye umri wa miaka 27 aliyejiunga na Chelsea akitokea klabu ya CSKA Moscow miaka miwili iliyopita, amesaini mkataba wa miaka minne na klabu ya Anzhi.

Mchezaji huyo ambaye alijiunga na Chelsea kwa kitita cha paundi milioni 18 na kucheza mechi 49 kwa klabu hiyo, alitambulishwa kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Anzhi ilipokuwa ikicheza mechi ya ligi dhidi ya Tom Tomsk siku ya Jumamosi.