Ngao ya Hisani Man United 3 Man City 2

Bao la Nani dakika ya 94 ya mchezo, liliiwezesha Manchester United kurejea katika mchezo kwa mtindo wa aina yake, ambapo hadi mapumziko walikuwa nyuma kwa mabao 2-0 na kufanikiwa kuwalaza mahasimu wao wakubwa wa mji mmoja Manchester City mabao 3-2 na kunyakua Ngao ya Hisani.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Manchester United wakishangilia Ngao ya Hisani

Huku kila mtu akiwa anajua mpambano huo utachezwa dakika 30 za nyongeza na hata ikibidi mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penalti, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno, aliivuruga ngome ya Manchester City na kutimua mbio kasi sana na kumzidi mlinzi Kompany baada ya kusogezewa pande kutoka kwa Wayne Rooney, akamzunguka mlinda mlango wa City Joe Hart na kuujaza mpira wavuni pasi na wasiwasi. Lilikuwa bao zuri la tatu na la ushindi kwa Manchester United.

City waliongoza kwa mabao 2-0 hadi wakati wa mapumziko baada ya mlinda mlango mwanagenzi wa United, Mhispania David De Gea kuonekana akibabaika na kushindwa kuucheza mpira wa juu wa krosi, hali iliyomfanya Joleon Lescott kupachika bao kwa kichwa na pia bao la pili la mkwaju wa mbali uliopigwa na Edin Dzeko.

Lakini United, wakiwa wanajua mechi zao mbili za mwisho katika uwanja wa Wembley walipoteza, kufungwa na Barcelona katika fainali ya Ubingwa wa Ulaya, pia kulazwa na Manchester City katika nusu fainali ya kombe la FA, walibadilika na kujipanga vizuri na kuweza kuwanyima raha majirani wao na hatimaye wakarejesha mabao mawili haraka haraka.

Chris Smalling alikuwa wa kwanza kupunguza deni la mabao, baada ya kuunganisha mkwaju wa adhabu ndogo uliochongwa na Ashley Young kabla Nani kusawazisha kabla ya kuandika bao la tatu dakika ya mwisho ya mchezo.

Kwa uhaki vijana wa Sir Alex Ferguson walipoteana wakati Manchester City walipofunga mabao yao ya haraka, huku winga wao mpya Young akionekana kuzoea mazingira mapya.

Manchester City, kwa upande mwengine walikuwa wakitumia vyema kila idara uwanjani na walichokusudia katika kipindi cha kwanza ni kumfanya mwamuzi Phil Dowd awe na kibarua kigumu, huku mlinzi Micah Richards akiwa miongoni mwa wachezaji wanne waliooneshwa kadi ya manjano kwa kumchezea vibaya Young.