Waziri arudi nyumbani kuangalia hali

Waziri wa Mambo  ya  ndani  wa  Uingereza Haki miliki ya picha PA
Image caption Waziri wa Mambo ya ndani wa Uingereza

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Theresa May amekatiza likizo yake na kurejea nyumbani kufuatia usiku wa pili wa ghasia mjini London.

Zaidi ya watu 100 wamekamatwa na maafisa 35 wa Polisi kujeruhiwa, magari ya Polisi pia nayo yameharibiwa na maduka kuporwa katika sehemu nyingi za mji.

Ghasia za Tottenham za siku ya Jumamosi ziliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa London kama vile Enfield na Walthamstow na mji wa Brixton ulio kusini mwa London.

Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg ametaja ghasia hizo kuwa wizi wa kunyatia.

Theresa May, ambaye amekuwa akiwasiliana na wanasiasa wengine wa ngazi za juu na wakuu wa Polisi akiwa nje ya nchi atakutana na kaimu kamishna wa Polisi Tim Godwin na maafisa wengine.

Hapo awali alisema kuwa Polisi kwa mara nyengine tena hapo jana walijiweka katika hatari kuwalinda wakazi wa mji wa London na mali yao.

Jumapili usiku maafisa watatu wa Polisi walijeruhiwa wakati gari moja lilipowagonga walipokuwa wanajaribu kuwakamata watu katika eneo la Waltham Forest.

Ghasia nyengine zilizuka katika eneo la Enfield ambako madirisha ya maduka yalivunjwa na gari la Polisi kuharibiwa.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Jumba lateketezwa Tottenham

Ghasia za Tottenham zilianza jumamosi usiku na kuendelea hadi jumapili asubuhi.

Maandamano ya amani kupinga mauwaji ya Mark Duggan mwenye umri wa miaka 29 ambaye alipigwa risasi na Polisi siku ya Alhamisi yalifuatiwa na ghasia nyakati za jioni.

Vurugu hizo zilienea katika mji ya karibu ya Wood Green na Tottenham Hale.

Naibu Waziri Mkuu ameeleza kuwa usiku wa pili wa mfululizo wa ghasia na vurugu ulitumiwa kupora mali na kuleta machafuko ambayo hayakuwa na uhusiano wowote na kifo cha Mark Duggan.