Saudi Arabia yamuondoa balozi wake Syria

Mizinga ya kijeshi Syria Haki miliki ya picha Reuters

Katika hatua ya karibuni kutoka jamii ya kimataifa dhidi ya Syria, Utawala wa Saudi Arabia umetaka serikali hiyo kukoma kuwalenga waandamanaji ambapo pia imetangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Damascus.

Taarifa ya Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia imesomwa kupitia runinga maarufu ya kiarabu ya Al Arabiya ambapo balozi wa Saudia ameitwa nyumbani kutoka Syria.

Katika kile kimeonekama kama hatua ya pamoja, muungano wa nchi za kiarabu umetoa taarifa yake rasmi iliyolaani machafuko nchini Syria.

Muda mfupi baadaye ikatolewa taarifa kali kutoka kwa mfalme Abdullah wa Saudi Arabia kupitia runinga ya kiarabu Al Arabiya.

Wadadisi wamesema taarifa hiyo ilinuia kuwafikia raia wengi wa Syria kupitia runginga hiyo, na milki nzima ya kiarabu ikiwa ni kilele cha mwezi wa Ramadhani.

Mfalme Abdullah ameitaka Syria kusitisha mauaji ya raia kiholela mara moja kabla hali kuzorota zaidi.Taarifa iliendelea kusema kinachoendelea Syria hakikubaliki popote hasa na Saudi arabia.

Mfalme ameonya Syria kutafakari vitendo vyake au ikumbwe na hasara kubwa.Taarifa hii imetokea wakati jeshi la Syria limeripotiwa kuwaua raia wengine hamsini.

Lalama dhidi ya mauaji ya raia huko Syria pia zilitolewa na papa pamoja na balozi wa Marekani mjini Damascus.Taarifa ya sasa imetajwa kama msimamo mpya wa Saudi Arabia ambayo imekuwa ikitetea uhuru wa nchi kutoingiliwa na dola za nje.

Na hii ni ishara ya shinikizo zaidi dhidi ya rais Bashar Al Asaad kutoka kwa jamii ya kimataifa.