Mashtaka yote dhidi ya Besigye yafutwa

Kizza Besigye Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kiongozi wa upinzani Kizza Besigye

Mahakama moja ya Uganda imefutilia mbali mashtaka yote yaliowasilishwa dhidi ya kiongozi wa upinzani Kizza Besigye yaliohusiana na maandamano kuhusu ongezeko la bei za bidhaa.

Alikamatwa mara nne na kushtakiwa kwa kuchochea ghasia wakati wa maandamano ambapo raia wa Uganda walihimizwa kutembea kwa miguu kwenda kazini.

Katika tukio moja Besigye alipigwa na Polisi jambo ambalo lilichochea maandamano. Makundi yakutetea haki za bindamu walilaani kukandamizwa waandamanaji, wakati huo inasemekana watu tisa waliuawa.

Bw Besigye alishindwa katika uchaguzi wa rais wa mwezi February lakini anadai uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura.

Serikali imemshutumu Bw Besigye kwa kujaribu kuiga mapinduzi ya Misri na kutaka kupata uwongozi kupitia fujo za barabarani baada ya kushindwa katika uchaguzi.

Hakimu George Wetyekere amefutilia mbali mashtaka matatu dhidi ya Bw Besigye ambayo yalihusu kukiuka sheria, kufanya ghasia na vile vile kuchochea ghasia. Mashtaka mengine ya kuchochea ghasia yalikuwa tayari yamefutwa.

Hakimu pia alisisitiza kuwa umma unahaki ya kufanya maandamano. Bw Besigye alikwenda hadi Kenya kupata matibabu baada ya kupigwa na kupuliziwa hewa iliyokuwa na pilipili.

Bw. Besigye amesema mashtaka hayo yalikuwa na msukumo wa kisiasa. Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2006 alishtakiwa kwa uchochezi na ubakaji lakini baadae aliachiwa huru.

Alikuwa wakati mmoja Daktari wa Rais Yoweri Museveni lakini wakahasimiana.

Bw Besigye aliondoka Uganda akisema maisha yake yako hatarini, lakini alirudi nyumbani mwaka 2005 kulipotangazwa sera ya vyama vingi vya siasa.