Bunge Uingereza laitwa kujadili ghasia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bunge la Uingereza kujadili ghasia

Bunge la Uingereza limeitwa kukutana siku ya Alhamis kufuatia machafuko yanayoendelea nchini humo, Wazri Mkuu amesema.

Kamati ya mambo ya dharura ya serikali ilikutana Jumanne baada ya ghasia kusambaa mjini London, na katika miji mingine mikubwa.

"Tutafanya kila linalowezekana kurejesha utulivu katika mitaa ya Uingereza na kuifanya salama kwa kufuata," Waziri Mkuu alisema nje ya Downing Street.

Zaidi ya maafisa 16,000 watakuwa katika mitaa ya London siku ya Jumatano, alisema

Takriban watu 450 wamekamatwa mpaka sasa, Bw Cameron alisema.

Aliwaambia wafanya ghasia, "Nguvu kamili ya sheria itawafikia", alisema watu wanatakiwa "kushirikiana pamoja kulaani uhakifu huu ".

Waziri mkuu alirejea mapema baada ya kusitisha likizo yake kujadili machafuko hayo, ambayo yalianzia siku ya Jumamosi baada ya maandamano ya amani eneo la Tottenham kutokana na polisi kumuua kwa risasi mtu mmoja.

London imeshuhudia wimbi la "uhalifu wa kuaga " katika siku tatu zilizopita, polisi wa London wamesema. Zaidi ya watu 69 wameshtakiwa kwa makosa mbalimbali baada ya mamia kukamatwa.

Birmingham, Liverpool, Nottingham na Bristol ni miongoni mwa miji mingine iliyokumbwa na ghasia hizo.

Naibu Kamishna Msaidizi wa Polisi Steven Kavanagh alisema ilikuwa "inatisha na inasikitisha London kuamkia asubuhi ya aina hii ".

"Polisi walijikuta wana kazi kubwa kuliko kawaida hali ambayo haijawahi kutokea," alikiambia kipindi cha BBC asubuhi.

Kaimu Kamishna Tim Godwin alitupilia mbali jeshi kuingilia kati kusaidia kupambana na ghasia hizo, lakini alisema: "Tutakwenda kila mahali kwa idadi kubwa zaidi usiku."