Afrika Kusini yaidhinisha bima ya afya

Jacon Zuma rais wa Afrika Kusini

Afrika Kusini imepiga hatua katika kuimarisha afya ya umma, baada ya serikali kuridhia bima ya afya ya kitaifa.

Bima hii inanuia kumwezesha kila raia wa Afrika Kusini kupata matibabu.

Waziri wa afya Aron Motsoaledi ametangaza mpango huo wa bima ya afya baada ya baraza la mawaziri kuuwidhinisha kwenye kikao cha Jumatano. Umma utakubaliwa kutoa maoni yao juu ya bima hiyo kabla ya mswada wake kuwasilishwa bungeni.

Waziri huyo amesema bima hii itaanza kutekelezwa kwa awamu kwanzia mwaka ujao na kuendelea hadi miaka 14. Bima hii inatoa nafasi kwa maelfu ya raia masikini wa Afrika Kusini kuweza kupata huduma bora za matibabu, kwa gharama ya chini sana.

Chama tawala cha African National Congress{ANC} kinakadiria kwamba mpango huu utaigharimu serikali dola bilioni 18 na utafadhiliwa kupitia kodi za wananchi na mapato mengine ya serikali.

Wafanyikazi wanaopata kiwango fulani cha mishahara, watatozwa kodi maalum kufadhili bima ya afya ya umma. Mfumo wa afya Afrika Kusini umetajwa kuwa wa viwango vya chini sana. Hospitali za umma zimefurika wagonjwa bila kuwepo huduma za kutosha za madaktari na wauguzi.

Serikali inatumaini kwamba bima mpya itabadilsha taswira ya sekta yake ya afya ambapo asili mia 80 ya raia wanategemea huduma katika hospitali na sahanati za umma.