Msaada utalindwa Mogadishu

Waziri Mkuu wa Somalia ametangaza kuanzishwa kwa kikosi maalumu cha kulinda misafara ya chakula cha msaada kinachopelekwa kwa watu waliokumbwa na ukame na njaa.

Haki miliki ya picha AP

Abdiweli Mohamed Ali alisema kikosi cha awali cha askari 300 piya kitalinda makambi ya wakimbizi mjini Mogadishu.

Alisema hayo baada ya kukutana na mratibu wa msaada wa dharura wa Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, ambaye amekuwa akizuru Somalia.

Bi Amos alisema, kwa vile usalama umetengenea Mogadishu, inamaanisha kuwa Umoja wa Mataifa unaweza kusaidia watu wengi zaidi mjini humo.

Umoja wa Mataifa unasema watu kama milioni 12 wameathiriwa na ukame na njaa katika Pembe ya Afrika.