Washukiwa wa ghasia mahakamani Uingereza

Ghasia Uingereza
Image caption Ghasia Uingereza

Mwanamume wa miaka 26 na kijana wa miaka 17, wameshtakiwa kwa mauaji ya wanaume watatu ambao waligongwa na gari mjini Birmingham katika ghasia za juma lilopita nchini Uingereza.

Haroon Jahan, Shazad Ali na Abdul Musavir walipondwa katika mtaa wa Winson Green wakati wanalinda maduka yasiporwe wakati wa ghasia.

Leo jioni kunafanywa mhadhara wa amani katika mji huo wa Birmingham, na maelfu ya watu wanatarajiwa kuhudhuria.

Joshua Donald mwenye umri wa miaka 26 na kijana wa miaka 17, ambaye kisheria hawezi kutajwa jina wanafikishwa mahakamani mjini Birmingham leo, kila mmoja anakabili mashtaka ya kuuwa watu watatu.

Leo pia mhadhara wa amani utaowakilisha jamii zote, utafanywa katika mtaaa wa Winson Green.

Watu wa madhehebu mbalimbali watawakilishwa na viongozi wao wa kidini.

Shughuli hiyo imeungwa mkono na serikali ya jiji.

Inakisiwa watu kama elfu-20 watahudhuria.

Na mjini London peke yake watu zaidi ya 1,200 wamekamatwa kwa kuhusika na ghasia.

Mkuu wa kikosi cha polisi cha Scotland Yard, anafikiri idadi itaongezeka.

Mahakama kadha yasiyowahi kufanya kazi Jumapili, leo yatafunguliwa kusikiliza kesi nyingi zilioko.

Wizara ya Sheria inasema, haikupata kuwa na mrundiko wa kesi namna hivi.