Baba yake Obi Mike hajulikani alipo

Baba yake mchezaji wa timu ya taifa ya Nigeria na klabu ya Chelsea, John Mikel Obi ametekwa nchini Nigeria.

Image caption John Obi Mikel

Bwana Michael Obi hajaonekana wala kusikika tangu aliposhindwa kurejea nyumbani kwake akitokea kazini siku ya Ijumaa katika mji wa Jos, mji mkuu wa jimbo la Kati ya Nigeria la Plateau.

"Baba yake John Mikel Obi ametekwa nchini Nigeria siku ya Ijumaa," Shirika la SEM Group lilitangaza katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

John Obi Mikel mwenyewe alifahamishwa juu ya kutekwa kwa baba yake kabla ya mechi ya Jumapili ya Ligi Kuu ya Soka ya England, ambapo Chelsea ilitoka sare na Stoke City, lakini aliamua kucheza.

SEM imesema hakuna fedha za kikombozi zilizotolewa hadi sasa na kwamba Mikel aliamua kucheza mechi hiyo "ili asiiangushe timu yake na familia yake".

Familia yake iliiambia BBC kwamba hawana mawasiliano na Mzee Obi lakini wanaamini "yu salama na mwenye afya njema".

Wakala wa mchezaji huyo wa Chelsea John Ola Shittu, amesema kila mmoja katika familia yake ana matumaini.

"Ni hali ngumu kwa John," alisema Shittu.

"Familia yake iliyopo mjini Jos ilitoa ripoti ya kupotea kwake katika kituo cha polisi kama ilivyotakiwa, lakini tunachukua hatua zote muhimu kumsaka."

Shittu amesema familia ya Mikel bado haijasikia chochote kutoka kwa yeyote akidai kumshikilia Mzee Obi.

Utekaji nyara hutokea zaidi nchini Nigeria kwa wafanyakazi wa mafuta, watu matajiri na maarufu.

Wacheza kandanda na familia zao wanazidi kulengwa na watekaji nyara.

Mwezi wa Julai mwaka 2008, kaka yake mlinzi wa timu ya Taifa ya Nigeria na Everton Joseph Yobo, alitekwa katika mji wa Port Harcourt, ambapo watekaji nyara walidai walipwe fedha.

Haijafahamika iwapo fedha za kikombozi zilitolewa au la, lakini Nornu Yobo aliachiliwa baada ya kushikiliwa kwa karibu wiki mbili.