FA yazishtaki Newcastle na Arsenal

Newcastle na Arsenal zimeshtakiwa na Chama cha Soka cha England- FA kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wao katika mechi yao waliyocheza siku ya Jumamosi ya Ligi Kuu ya England.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Barton akishikana na Gervinho

Mshambuliaji wa Gunners, Gervinho alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 76 baada ya kukamatana mashati na kusukanasukana na Joey Barton.

Barton alimuinua Gervinho kwa hasira alipoanguka na kumshutumu kwamba alijiangusha na Gervinho akamzaba kibao Barton, hali iliyosababisha atolewe nje kwa kadi nyekundu.

Kiungo wa Arsenal Alex Song pia ameshtakiwa kwa kitendo cha vurugu baada ya patashika na Barton.

Arsenal tayari imekata rufaa dhidi ya kadi nyekundu aliyooneshwa Gervinho ambayo itamfanya asicheze mechi tatu, zikiwemo mechi dhidi ya Liverpool na Manchester United.

Taarifa iliyotolewa na FA imesema: "Newcastle United na Arsenal zimeshtakiwa na FA kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wao kufuatia mechi ya Jumamosi katika uwanja wa St James' Park.

"Klabu zote mbili zimeshtakiwa kufuatia mzozano uliohusisha wachezaji wengi ambapo baadae Gervinho wa Arsenal alioneshwa kadi nyekundu katika dakika ya 75.

"Kufuatia kutolewa nje kwa Gervinho, Arsenal imepeleka malalamiko kwamba adhabu ya kawaida kukosa mechi tatu ni kali mno. Tume ya Nidhamu itasikiliza shauri hilo.

"Wakati huo huo Alex Song kiungo wa Arsenal ameshtakiwa na FA kwa makosa tofauti kutokana na tukio lililotokea katika mechi hiyo hiyo.

"Klabu zote mbili zimepewa muda hadi tarehe 18 Agosti saa kumi jioni kujibu mashtaka yao, wakati Song anatakiwa hadi tarehe 16 saa kumi na mbili jioni kujibu tuhuma zinazomkabili."

Katika taarifa yao klabu ya Newcastle imekanusha mashtaka yanayowakabili.

Barton, yeye alioneshwa kadi ya manjano katika mkwaruzano na Gervinho.