Petr Cech nje kwa wiki nne

Kipa wa Chelsea Petr Cech hatoweza kucheza kwa wiki tatu hadi nne baada ya kuumia goti akiwa mazoezini.

Image caption Petr Cech

Cech, 29, atakosa mechi za ligi kuu dhidi ya West Brom, Norwich, Sunderland na Manchester United.

Meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas atalazimika kuchagua kati ya Hilario au Ross Turnbull, ambao ni makipa wa akiba.

Kipa mwingine wa akiba aliyesajiliwa hivi karibuni na Chelsea Thibault Courtois anachezea Atletico Madrid kwa mkopo.

"Alianguka vibaya, tulidhani ameumia sana," amesema Villas-Boas.

Ameongeza: "Ilikuwa mwisho wa kufanya mazoezi, na ni jambo ambalo hutokea mazoezini."

Cech pia atakosa mchezo wa ufunguzi wa Chelsea wa Klabu Bingwa Ulaya, na pia mchezo wa timu yake ya taifa wa kufuzu kucheza Euro 2012 dhidi ya Scotland.

"Tutaamua siku ya Ijumaa nani atakuwa kipa. Tuna makipa wawili, mmoja ataanza na mwingine atakuwa wa akiba." amesema meneja wa Chelsea.