ANC ya Afrika Kusini kumuadhibu Malema

Image caption Julius Malema, kiongozi wa Vijana wa ANC

Mkutano mkuu wa chama tawala cha ANC nchini South Africa umeamua kumuadhibu kiongozi wa vijana Julius Malema kwa kuchafua sifa ya chama hicho.

Tuhuma za hivi karibuni zinatokana na kauli zake kuwa Umoja wa Vijana wa ANC utafanya uwezalo kuanzisha mabadiliko ya utawala wa nchi jirani ya Botswana.

Bw Malema alikuwa ‘akipanda mbegu za mgawanyiko’ ndani ya chama, ANC imesema.

Ni kiongozi mashuhuri Afrika Kusini lakini maoni yake kuhusu kutaifisha madini na mashamba yamesababisha hisia tofauti kutoka kwa umma.

"Komredi Julius Malema amekuwa akituhumiwa kwa matukio kadhaa ya kuvunja katiba ya ANC ikiwemo kuiingiza ANC katika migogoro kupitia kauli na matamshi yake kuhusu Botswana na kupanda mbegu za mgawanyiko katika uongozi wa Chama," Chama hicho kilisema katika taarifa yake.

ANC kinasema suala lake sasa limo mikononi mwa Kamati ya Maadili ya ANC, ambayo itaamua tarehe, mahali na muda wa kusikiliza tuhuma hizo.

Mapema wiki hii, Bw Malema amekiomba radhi ANC kwa kusema kuwa utawala wa serikali ya Botswana ni wa vibaraka na ni tishio kwa Afrika.