Stoke yalazimisha sare 1-1 na Norwich

Bao la kusawazisha dakika za nyonge kipindi cha pili lililofungwa na Kenwyne Jones liliinyima ushindi Norwich iliyokuwa ikicheza pungufu ya mchezaji mmoja katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya England kuchezwa uwanja wa Norwich wa Carrow Road kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.

Image caption Kenwyne Jones

Norwich walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 37 baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Ritchie De Laet kumpita mlinda mlango wa Stoke Asmir Begovic.

Leon Barnett alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia rafu Jon Walters, rafu iliyosababisha kupigwa mkwaju wa penalti uliookolewa na mlinda mlango John Ruddy.

Lakini Jones, aliyesajiliwa kutoka Sunderland mwaka 2010, alivunja matumaini ya Norwich kwa kupachika bao la kichwa tena katika dakika za majeruhi.

Nayo Wolves imeendelea kumajiimafrisha na kupata ushindi wa pili mfululizo msimu huu baada ya kuilaza Fulham mabao 2-0.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kevin Doyle akichanja mbuga

Bao la kwanza la Wolves lilipachikwa katika dakika ya 42 baada ya kazi nzuri ya Kevin Doyle kwa mkwaju maridadi kabla ya Matt Jarvis kumalizia kazi na kufunga bao la pili dakika moja kabla ya mapumziko.

Matokeo hayo yanaifanya Wolves kushikilia nafasi ya pili nyuma ya Manchester City wote wakiwa na pointi sita.

Manchester City ikicheza mtindo wa kushambulia kwa kasi msimu huu ilifanikiwa kuilaza Bolton mabao 3-2 nyumbani kwao katika mechi iliyokuwa ya kusisimua.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Edin Dzeko

David Silva aliipatia City bao la kwanza kwa mkwaju wa pembeni mwa sanduku la hatari la Bolton wakati mlinda mlango Jussi Jaaskelainen akiwa hajajiandaa na kupishana na mpira ukiwa unaelekea wavuni.

Gareth Barry baadae akaachia mkwaju wa mbali na kuipatia City bao la pili kabla ya Ivan Klasnic kufufua matumaini ya Bolton kwa kuandika bao la kwanza kutokana na pande la pembeni kutoka kwa Martin Petrov.

Manchester City walionekana kuendelea kudhibiti mchezo baada ya Edin Dzeko kuanchia mkwaju katika dakika ya pili tu ya kipindi cha pili akiwa ndani ya sanduku la lango la Bolton na kuandika bao la tatu na licha ya Kevin Davies kuifungia Bolton bao la pili kwa kichwa, bado City waliendelea kumiliki mchezo zaidi.

Sergio Aguero wa Manchester City angeweza kufunga mabao kwa urahisi mara mbili baada ya kupatiwa mpira na Dzeko, lakini alipiga mkwaju uliopaa na baadae kichwa alichopiga mpira ukatoka nje sentimita chache ya lango la Bolton.

Kwa ujumla lilikuwa pambano la kuvutia sana huku wachezaji wa Manchester City wakionana kwa pasi murua na kufanikiwa kuipenya ngome ya Bolton mara kwa mara.

Carlos Tevez aliyekuwa mchezaji wa akiba hatimaye aliingia kuchukua nafasi ya Aguero, lakini namna Dzeko, Aguero na Silva walivyokuwa wakionana kunampatia meneja wa City Roberto Mancini matumaini ya kufanya vizuri kwa timu yake msimu huu, hata kama Tevez ataondoka au la.