Graham amtaka Wenger kusajili haraka

Meneja wa zamani wa Arsenal George Graham, amesema Arsene Wenger anahitaji kuwa na wachezaji wenye mbinu tofauti iwapo anahitaji tena kushinda vikombe.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wenger akitoka uwanjani baada ya kufungwa na Liverpool

Akizungumza katika kipindi cha michezo ya wiki cha Radio 5, Graham amesema Arsenal itakuwa na kibarua kigumu iwapo itahitaji kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi msimu huu.

"Wanaonekana hawako imara. Kila mmoja alikuwa anafahamu Fabregas ataondoka," alisema.

"Siamini kama hawajapata mtu wa kuziba nafasi ya Fabregas. Wanahitaji wachezaji wenye uzoefu kuwasaidia vijana hodari walionao."

Graham amempongeza Wenger kwa kushinda mataji mara tatu, lakini akasema kikosi cha sasa ni tofauti kabisa na kile kilichokuwepo msimu wa 2003-04 ambacho hakikupoteza mchezo hata mmoja katika mechi zote 38 za Ligi Kuu ya Soka.

Wenger anazo pesa alizouzia wachezaji akina Cesc Fabregas aliyejiunga na Barcelona, pamoja na Gael Clichy aliyehamia Manchester City na Emmanuel Eboue aliyekwenda Galatasaray.

Mipango ya Samir Nasri kuhamia Manchester City bado ipo hai, licha ya taarifa za mazungumzo kukwama baina ya vilabu hiyvyo viwili.

Graham aliendelea kueleza, "Nadhani wanahitaji wachezaji wengine watatu katika kikosi cha sasa.

Alimtafadhalisha Wenger: "Tafadhali toa pesa. Ninachoona wanahitaji mlinzi wa kati mwengine, kiungo mwenye uzoefu na bado wanahitaji mshambuliaji mwenye kukaribia au kuzidi uchezaji wa Thierry Henry.

Arsenal msimu huu wameweza kumnunua mshambuliaji Gervinho kutoka Lille, na chipukizi wa kutumainiwa Joel Campbell, Carl Jenkinson na Alex Oxlade-Chamberlain.