Waasi wavamia makazi ya Gaddafi

Waasi wa nchini Libya wameiteka ngome yenye makazi ya Kanali Muammar Gaddafi mjini Tripoli, mojawapo ya maeneo ya mwisho chini ya udhibiti wa kiongozi huyo.

Image caption Waasi katika mitaa ya Tripoli

Picha za televisheni zimeonyesha wapiganaji wakiangamiza masanamu kadhaa mkiwemo sanamu la Kanali Gaddafi na kufyatua risasi hewani huku wakishangilia wakiwa ndani ya makao hayo.

Makamanda wa waaasi waliyalenga majengo hayo ambayo yalikua ndiyo nembo kuu ya utawala wa Gaddafi.

Haijajulikana kama Kanali huyo ama jamaa yake yoyote walikuwemo katika makao hayo ya Bab al-Aziziya.

Ngome

Wapiganaji waliokuwa na silaha nzito nzito walimiminika katika jiji la Tripoli Jumaanne asubuhi kushiriki katika shambulio hilo dhidi ya ngome hiyo ambayo waasi wanaamini ndio hatua itakayomaliza mapambano haya.

Wanahisi wakishika udhibiti wa makao haya au kumuua Kanali Gaddafi basi nchi nzima itakua mikononi mwao.

Mtandao

Hakukua na ishara zozote za upinzani licha ya ripoti za mamia ya wafuasi wa Gaddafi kupewa jukumu la kuyalinda makao haya

Inaaminiwa kuwa makao ya Bab al-Aziziya yana mtandao mkubwa wa mahandaki yanayounganisha maeneo kadhaa muhimu ya jiji la Tripoli.

Kuna majengo ya wanajeshi, maskani kuu ya Kanali Gaddafi, maktaba na ofisi za serikali.

Mwaandishi wa BBC Rana Jawad akiwa Tripoli anasema kuna hali ya msisimko mkubwa kwamba huu ndio mwisho wa Kanali Gaddafi lakini sherehe hasa hazitaanza mpaka pale yeye na familia yake watakapopatikana.