Jumuiya ya kimataifa na hali halisi Libya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague na viongozi kwenye mkutano Doha, Qatar

Jamii ya kimataifa inaendelea kujirekebisha kukabiliana na hali halisi nchini Libya.

Nchi kadhaa zimelitambua baraza la taifa la mpito kua ndio mamlaka halali nchini Libya.

Miongoni mwao ni mataifa ya Afrika ambako Libya imechangia vilivyo hata kama si kwa manufaa ya mataifa mbali mbali .

Muuungano wa Afrika(AU) ambao ulijaribu kuwa mpatanishi katika Libya bado haijalitambua baraza la taifa la mpito kuwa ni wawakilishi halali wa Libya.

Nourridine Mezz msemaji wa halmashauri kuu ya utawala wa AU anasema tangu mwanzo walizungumzia kuwepo kipindi cha mpito kitakachojumuisha pande zote ili wananchi wa libya wafikie malengo yao ya demokrasia,uhuru na uwazi. "Tumekuwa tukitafuta suluhisho madhubuti na la amani .

Inasikitisha kwamba tulipuuzwa. Libya iko barani Afrika kwa hiyo ni jukumu letu kuendelea kuwasaidia wananchi wa Libya kutoka janga hili halikadhalika wafanyikazi Waafrika ambao wamekwama huko.

Tunafanya hivyo lakini hatimae hatima ya Gaddafi na nani anaongoza Libya ni kwa wananchi wa Libya kuamua"

Lakini baadhi ya nchi za Kiafrika zimeamua kuvunja mshikamno wa AU kwa kulitambua baraza la mpito kuwa ndio wawakilishi halali.

Hawa ni pamoja na Senegal,Gambia ,Morocco, Niger na Misri. Nigeria ambayo ndio yenye wakaazi wengi kupita wote barani Afrika nayo pia imechukua hatua kama hizo.

Lakini taifa hili kuu la Afrika linataka viongozi wapya - waunde utawala unaowakilisha matabaka yote na kuitisha uchaguzi huru na wa haki.

Huo ndio msimamo pia wa Kenya ingawa bado haijalitambua rasmi baraza la utawala wa mpito.

Lakini kuna nchi kama Ghana ambazo bado zinachunguza kabla ya kuamua hatua gani zichukuliwe.

Inaelekea huu ndio msimamo wa taifa linaongoza kiuchumi barani Afrika--Afrika ya kusini ambayo imezihimiza nchi za Afrika zisikurukupie mambo tu hasa ikizaingatiwa AU inafanya mkutano wake wiki hii.

Afrika ya Kusini iliongoza juhudi za Afrika kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa mgogoro wa Libya. Hivi sasa wameitisha mazungumzo ya kisiasa kati ya baraza la mpito na serikali ya Muammar Gaddafi.

A.Kusini pia inahisi mashambulio ya NATO yalikiuka idhini ya Umoja wa mataifa ya kuwalinda raia.Na hii ilivuruga juhudi za Afrika kutafuta suluhisho la amani.