Joice ataka kifo cha mumewe kichunguzwe

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jenerali Mujuru na mkewe Joice Mujuru

Makamu wa Rais wa Zimbabwe Joice Maimu ametoa wito wa kufanywa uchunguzi wa kifo cha mume wake Solomon kilichotokea wiki iliyopita kwenye shamba lao.

Aliyekuwa mkuu wa majeshi, Jenerali Mujuru alikuwa ni mtu mwenye ushawishi mkubwa kwenye chama cha Robert Mugabe cha Zanu-PF.

Mwandishi wa BBC alisema kifo chake kimeibua wasiwasi kuwa huenda aliuliwa, na kusababisha mpasuko ndani ya chama na zahama juu ya atakayemrithi Bw Mugabe.

Bi Mujuru alisema nyumba hiyo yenye milango chungu nzima ya kutokea kunamaanisha ilikuwa rahisi kwake kuukimbia moto huo.

Rex Nhongo

Bw Mujuru mwenye umri wa miaka 62, alikuwa mwanasiasa mwandamizi na mume wa Makamu wa Rais wa Zimbabwe Joice Mujuru.

Wachambuzi wanasema kifo chake huenda kitazidisha mkanganyiko kwenye chama cha Rais Mugabe kuhusu nani atakayemrithi kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 87.

Akijulikana kama Rex Nhongo wakati wa vita vya msituni, alikuwa mkurugenzi wa vikosi vya Mugabe wakati wa vita vya uhuru miaka ya 70.

Afisa mmoja ameiambia BBC kuwa Jenerali Mujuru alikufa kwa moto uliotokea katika nyumba yake ya shambani katika eneo la Beatrice, kilometa 80 (maili 50) kusini mwa mji mkuu Harare asubuhi ya Jumanne.

Haijulikani iwapo alikuwa peke yake wakati huo au kama alipewa ulinzi wa jeshi.

Mwandishi wa BBC Brian Hungwe mjini Harare anasema Jenerali Mujuru alikuwa mwanachama mwandamizi wa chama cha Zanu-PF na anaelezwa kuwa alikuwa mwenye msimamo wa kadri.

Alikuwa mpanga mikakati na kusemekana akiwa na ushawishi mkubwa wa kuweka viongozi wenye nguvu katika siasa za Zanu-PF , anasema.

Kifo chake kimeacha pengo na kumuuacha mkewe bila nguzo ambaye ni mmoja kati ya makamu wawili wa Rais, wachambuzi wanasema.

Wakati wa vita dhidi ya utawala wa Rhodesia katika miaka ya70, Jenerali Mujuru aliongoza mapambano ya silaha pamoja na marehemu Josiah Tongogora.

Mwandishi wa BBC anasema ni Jenerali Mujuru aliyewahamasisha wapigania uhuru wa Msumbiji wakati wa mgogoro kumkubali Bw Mugabe kama kiongozi wa vikosi vya vuguvugu la waasi wa Zanla baada ya kuachiliwa kutoka kizuizini mwaka 1974.

Wakati wa uhuru mwaka 1980 aliongoza kikosi cha jeshi kabla ya kustaafu na kuingia katika biashara miaka 10 baadaye.