Adebayor aenda Tottenham

Tottenham imethibitisha kumsajili mshambuliaji Emmanuel Adebayor kwa mkopo hadi mwisho wa msimu kutoka Manchester City.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Emmanuel Adebayor

Mapema wiki hii meneja wa Tottenham Harry Redknapp alithiibitisha kuwa klabu yake iko katika mazungumzo na City kuhusiana na uhamisho wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27.

Adebayor hakuwa kipenzi cha meneja wa Man City, Roberto Mancini mwaka jana, na hivyo kupelekwa Real Madrid kwa mkopo.

Spurs pia wamemsajili kiungo kutoka Uhispania Yago Falque kutoka Juventus ya Italia.

Spurs na City wamekuwa wakizungumza kwa muda kuhusiana na mkataba wa Adebayor, huku ikiripotiwa kuwa mshahara wake wa pauni 170,000 kwa wiki ukiwa ndio kikwazo kikubwa.

Mancini aliweka wazi kwa mshambuliaji huyo kutoka Togo, aliyejiunga na City akitokea Arsenal kuwa hana nafasi kubwa kutokana na kuwepo kwa Carlos Tevez, Sergio Aguero, Mario Balotelli na Edin Dzeko.

Mwezi April Adebayor alisema angependa kusalia Real Madrid.

Adebayor alifunga mabao mawili dhidi ya Tottenham katika robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya wakati timu hizo zilipokutana kwenye uwanja wa Bernabeu msimu uliopita.