Sheik Sharif aibembeleza Puntland

Haki miliki ya picha NET
Image caption Sheik Sharif amepokewa Punland

Rais wa serikali ya mpito ya Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009 aliposhika uongozi, amewasili katika jimbo lililojitenga la Puntland , ambalo liko kaskazini mashariki mwa nchi ya Somalia.

Kwa muda sasa uhusiano kati ya Somalia na Puntland umekuwa sio mzuri, na katika siku za hivi karibuni tofauti mpya zimeibuka kati yao juu ya mkutano wa mashauriano juu ya mustakbala wa Somalia nzima unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Mogadishu.

Afisa katika ofisi ya rais wa Somalia ameiambia BBC kuwa ziara ya Rais Sharif inatokana ni juhudi za mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Somalia, Balozi Augustine Mahiga, ambaye anajaribu kuzileta pamoja pande hizo mbili ingawa hakutoa ufafanuzi zaidi.

Kutokana na tofuati za kikoo kutawala siasa za Somalia, jimbo hilo lililojitenga la Puntland kwa muda sasa limekuwa hazifurahii harakati za serikali ya mpito ya Somalia inayoongozwa na Sheik Sharif.

Uhamsa kati ya Somalia na Puntland yalianza kujitokeza baada ya aliyekuwa Rais wa serikali ya mpito Abdullahi Yusuf Ahmed ambaye ni kutoka Puntland kulazimishwa kujiuzulu mapema mwaka wa 2009, na nafasi yake kuchukuliwa na Rais Sharif kutoka Mogadishu.

Puntland na serikali ya Sheikh Sharif wamekuwa wakizozana pia juu ya ugavi wa rasilimali za kitaifa kama vile misaada kutoka nje na usimamizi wa mikataba ya uchimbaji mafuta na madini mengine.

Wakati mzozo ulivyoibuka ndani ya uongozi wa serikali ya mpito juu ya kumalizika kwa mhula wa serikali ya mpito wa Somalia , Rais Abdirahman Farole wa Puntland alikuwa msatari wa mbele kumpinga Rais Sharif ambaye alikuwa anataka serikali yale ya mpito iongezewe muda.

Lakini mambo yameanza kubadilika kidogo kidogo baada ya mkataba wa Kampala ulioipatia serikali ya mpito muda wa mwaka mmoja zaidi kuwa madarakani, na hatua iliyofuatia ya Rais Sharif ya kumteua waziri mkuu Abdiweli Mohamed Ali kutoka eneo la Puntland.

Haki miliki ya picha NET
Image caption Punland

Hata hivyo, mkutano wa mashauriano juu ya mustakbala wa Somalia unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao ndani ya Somalia unaaminika kusababisha tofauti mpya kati ya pande hizo mbili.

Serikali ya mpito ya Somalia inasisitiza kuwa mji mkuu Mogadishu ndio unafaa kuandaa majadiliano hayo wakidai kuwa Mogadishu sasa ni salama baada ya wanamgambo wa Kiislamu kufurushwa . Lakini Puntland kwa upande wake inasisitiza kuwa ndiyo inayofaa kupewa fursa ya kuandaaa mkutano huyo.