Sudan yatoa malalamiko Umoja wa Mataifa

Sudan imewasilisha malalamiko kwenye baraza la usalama la umoja wa mataifa, ikiishutumu taifa jipya la Sudan Kusini kwa kuwaunga mkono waasi kwenye mji wenye utajiri uliopo mpakani.

Awali, makundi ya kutetea haki za binadamu yaliishutumu Sudan kwa kurusha mabomu kwenye makazi ya raia Kordofan kusini, licha ya kutangaza kusitisha mapigano eneo hilo wiki iliyopita.

Haki miliki ya picha trevor snapp
Image caption Ghasia milima ya Nuba

Umoja huo umesema takriban watu 200,000 wamekimbia eneo hilo, ambapo Sudan imekataa mashtaka ya kuhusishwa na mauaji ya kimbari.

Wengi kutoka kabila la Wanubi walipigana na upande wa Kusini wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kipindi cha miongo miwili.

Baada ya uhuru wa Sudan kusini, walijikuta wakiongozwa na serikali ya Khartoum waliopigana nao kwa miaka mingi.

Ghasia hizo zilianza baada ya serikali ya Sudan ilipojaribu kuwanyang'anya silaha wapiganaji.

Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yameishutumu Sudan kwa kupiga mabomu kwenye maeneo waishio raia.

Ni vigumu kupata taarifa sahihi kutoka eneo hilo kwani waandishi wa habari na wanadiplomasia wamezuiwa kufika mjini hapo na umoja wa mataifa unakabiliwa na vikwazo.

Kordofan kusini ni mji pekee unaozalisha mafuta Sudan, kwani takriban asilimia 75 ya mafuta kwa ujumla yalikuwa yakitoka kwenye eneo ambalo sasa linatambulika Sudan kusini.