Libya yakataa vikosi vya UN

Utawala wa mpito nchini Libya umepinga fikra yoyote ya kutumia majeshi ya kimataifa, kwa mujibu wa mjumbe wa Umoja wa Mataifa aliye nchini humo.

Mjumbe Ian Martin amesema kuwa Umoja wa Mataifa ulikua na nia ya kutuma wasimamizi wa kijeshi nchini Libya.

Kabla ya hayo, Mwenyekiti wa baraza la mseto (NTC) alisema kuwa nchi hiyo haihitaji msaada kutoka nje kwa ajili ya kudhibiti hali ya usalama.

Habari hizo zinatoka wakati wapiganaji wanaotii baraza la mseto wakijiandaa kuingia mji alikozaliwa Gaddafi wa Sirte kutokea mashariki na magharibi.

Walinzi wa mji huo wamepewa hadi jumamosi kusalimu amri.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wa Libya washerehekea siku kuu ya Eid

Hata hivyo msemaji wa Kanali Gaddafi Moussa Ibrahim amepinga amri hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari.

Msemaji huyo alinukuliwa akisema kua "hakuna taifa duniani lenye heshima na hadhi iliyostahili ambalo lineweza kukubali amri ya magenge yenye silaha.

Bw.Ibrahim alikariri msimamo wa Kanali Gaddafi wa kumtuma mwanawe Saadi ili kujadiliana na waasi na kwa pamoja waunde serikali ya mseto. Shirika hilo limeongezea kusema.

Naibu Mwakilishi wa Libya kwenye Umoja wa Mataifa Ibrahim Dabbashi, ameiambia BBC kua hali nchini Libya ni hali isyo ya kawaida.

Naibu huyo amesema kua "umoja wa Mataifa umependekeza kutuma vikosi vyake vya walinzi wa amani nchini Libya lakini ukweli wa mambo ni kwamba mgogoro wa Libya una sura isiyo ya kawaida.

Hali halisi si ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, si mzozo baina ya makundi mawili, ila ni raia wanaojihami dhidi ya utawala wa kimabavu.

Hata hivyo, Bw.Martin amesema kuwa Umoja wa Mataifa unatarajia kuombwa kuunda kikosi cha polisi.

Baada ya Kikao maalum cha Umoja wa Mataifa, Bw.Martin akasema kua ni bayana kuwa wa Libya hawataki msaada wa aina yoyote wa kijeshi lakini kigezo kikuu kitakua ni jinsi gani Umoja wa Mataifa utaisaidia nchi hio katika kujiandalia uchaguzi wa kidemokrasi.

Ikumbukwe kuwa Libya haijawahi kuonja aina yoyote ya uchaguzi, hakuna mfumo wa aina yoyte ya uchaguzi, hawana tume ya uchaguzi hawajawahi kuwa na vyama vya kisiasa, hawana taasisi zilizo huru na vyombo huru vya habari ndiyo kwanza vimeanza kuchomoza huko mashariki mwa nchi katika siku za hivi karibuni.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema kuwa ongezeko la uhaba wa bidhaa zinazohitajika na watu ni suala linalohitaji hatua ya haraka na kulitaka baraza la usalama lijibu maombi ya baraza la mseto likitaka fedha za matumizi.

Ingawa shehena kubwa la dawa na chakula vilipatikana vilikofichwa na serikali siku chache zilizopita, tatizo kuu ni ukosefu wa maji.

Takriban asili mia 60 ya wakaazi wa mji wa Tripoli hawana huduma ya maji na hali ya usafi imetatizika.

Mnamo siku ya Ijumanne, Baraza la usalama la Umoja wa mataifa liliiruhusu Uingereza iachilie dinar bilioni 1.86 sawa na dola za kimarekani bilioni 1.55 kutoka mali zilizozuiliwa ili ziweze kutumika katika ununuzi wa bidhaa zinazohitajika nchini Libya. Hata hivyo juhudi kama hizo kutaka fedha za nchi hiyo takriban dola bilioni 8.6 zimezuiliwa na Ujerumani na Ufaransa.

Shirika la habari la Ufaransa, AFP limearifu kuwa Urussi inashikilia msimamo wa Ujerumani wa kukubali kutoa takriban dola bilioni 1.4 ya mali ya Libya iliyozuiliwa pamoja na msimamo wa Ufaransa wa kukubali kuruhusu takriban dola bilioni 7.2 za Libya kwa ajili ya kununulia msaada unaohitajika.

Wakati hayo yakiendelea Kanali Gaddafi hajulikani alipo, kukiwa natetesi kuwa labda yuko Sabha, Sirte au Bani Walid. Lakini naibu mkuu wa baraza la mseto, Ali Tarhouni amesema kuwa wanafahamu vyema alipo na kuongezea kuwa wana imani ya kumkamata mzima mzima.