Kiungo Scott Parker ajiunga na Tottenham

Tottenham imefikia makubaliano kumsajili kiungo wa timu ya taifa ya England Scott Parker kutoka klabu ya West Ham kwa kiticha cha karibu paundi milioni 5.

Image caption Scott Parker

Hatua hiyo imekuja baada ya Parker mwenye umri wa miaka 30 kuwasilisha maombi ya uhamisho siku ya Jumanne, akieleza anataka kucheza Ligi Kuu.

Kujiunga kwa Parker na timu hiyo ya kaskazini mwa London, huenda kumemfanya Wilson Palacios ajiunge na Stoke City.

Meneja wa Spurs Harry Redknapp alisema siku ya Jumatano kwamba Luka Modric hatahama klabu hiyo.

Parker, aliyejiunga na West Ham akitokea Newcastle kwa kitita cha paundi milioni 7 mwaka 2007, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Chama cha Waandishi wa Habari za Kandanda msimu uliopita, licha ya klabu yake kumaliza mkiani katika Ligi Kuu ya England.

West Ham imesema wamekubali "kwa shingo upande" kumuachia kiungo wao huyo, licha ya jaribio lao la kutaka kumbakisha Upton Park.