Wafuasi wa Gaddafi wapewa makataa

Viongozi wa mpito wa Libya wameyapa majeshi ya Kanali Muammar Gaddafi muda maalum wa kujisalimisha hadi Jumamosi la sivyo watakabiliwa na nguvu ya kijeshi.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waasi tayari kushambulia Sirte

Mustafa Abdul Jalil, ambaye analiongoza Baraza la Mpito la Libya (NTC), amesema muda huo maalum uliotolewa unawahusu askari watiifu kwa Kanali Gaddafi walio katika mji aliozaliwa wa Sirte na miji mingine nchini Libya.

Tamko hilo la waasi limetolewa baada ya mke wa Gaddafi na watoto wake wakubwa watatu kukimbilia nchi jirani ya Algeria.

Algeria imetetea hatua ya kuwapa hifadhi familia ya Gaddafi, hatua ambayo NTC imeita kuwa ni "kitendo cha uchokozi".

Majeshi yanayompinga Gaddafi yanajaribu kumaliza upinzani unaoendeshwa askari watiifu kwa Gaddafi, na kujiandaa kuingia mji wa Sirte.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Benghazi, Bwana Jalil amesema iwapo hakutakuwa na "dalili za kutekeleza kwa amani" amri hiyo ifikapo Jumamosi, "tutaamua suala hilo kijeshi".

Majeshi yanayompinga Gaddafi wanasema wataingia kijeshi kama kuyang'oa majeshi ya Gaddafi kama hawatafanikiwa kupoata kile wanachotaka kufikia Jumamosi.

Mwandishi wa BBC, Jon Leyne aliyeko Benghazi anasema majeshi ya waasi kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakijadiliana na viongozi wa kikabila katika miji ya Sirte mingine miwili mikubwa iliyobakia kuwa ngome za Gaddafi ya Bani Walid na Sabha, iliyopo katika jangwa la Sahara.