Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

MITA KWA MAKAHABA

Makahaba nchini Ujerumani wanatakiwa kununua tiketi maalum kutoka katika mita maalum wakati wakifanya shughuli zao katika mitaa mbalimbali nchini humo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mita mpya za makahaba

Makahaba katika jiji la Bonn watakabiliwa na faini kali kutoka katika mamlaka za mji iwapo watakutwa wakifanya shughuli zao bila kulipia.Nchini Ujerumani, wanawake wanaouza miili yao hutakiwa kulipa kodi ya mapato. Kiwango cha kodi hiyo hutofautiana kulingana na mji na mji.

Mita hizi mpya nchini Ujerumani zinaruhusu makahaba kununua tiketi kwa dola tisa ambayo itadumu kwa usiku mmoja. Msemaji wa jiji la Bonn amesema mita hizi zitahakikisha kodi inakusanywa bila tatizo lolote.

Iwapo kahaba atakamatwa akifanya shughuli zake bila tiketi, atawekwa rumande, na kukabiliwa na faini, na hata uwezekano wa kupigwa marufuku. Takriban makahaba mia mbili wanafanya shughuli zao mjini Bonn.

Kutokana na malalamiko kutoka kwa wakazi wa mji huo, maeneo maalum yametengwa kwa ajili ya shughuli hizo, na jiji pia limejenga mabanda ya mbao yaitwayo "maeneo ya mlo" ili wateja wenye magari waweze kujificha na makahaba.

KULA KULIPA

Bwana mmoja nchini Canada aliingia hotelini kula, na alipotakiwa kulipa, alimwambua mhudumu amsubiri kidogo. Bwana huyo alitoka hotelini na kwenda katika kituo kimoja cha kuuzia mafuta, na kuiba fedha, na kurudi na kulipia chakula chake.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Usisahau kulipa

Gazeti la Metro limesema bwana huyo Cory Henderson alikwenda kula katika hoteli ya Browns Kaskazini mwa Vancouver siku ya Ijumaa na kutakiwa kulipa dola thelathini na nane. Polisi wamesema wahudumu wa hoteli walipomtaka alipe fedha hizo, aliwajibu kuwa anatoka mara moja na atarejea baada ya muda mfupi.

Taarifa za polisi zimesema bwana huyo alikweda katika kituo cha mafuta na kumtishia muuzaji kwa kutumia screwdriver, na kisha kurejea hotelini na kulipa na fedha alizoiba. hata hivyo haijafahamika aliiba fedha kiasi gani.

Bwana Henderson sasa anashitakiwa kwa kosa la wizi, kujipatia chakula kwa njia za wizi, na kumiliki silaha hatari.

JESHI NA KITAMBI

Madaktari wa jeshi nchini Czech wamegundua kuwa nusu ya wanajeshi wa nchi hiyo wameota vitambi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Jeshi na kiriba tumbo.. wapi na wapi..

Shirika la habari la Reuters limesema jeshi hilo lina wanajeshi wapatao elfu ishirini na mbili. Taarifa zinasema nusu ya wanajeshi hao wana uzito uliozidi na wengine takriban elfu tatu na mia tano wana viriba tumbo.

Jeshi hilo limeamua kuchukua hatua za haraka maraka, ambapo wanajeshi watatakiwa kuacha kula, yaani kufanya diet. Taarifa zinasema jeshi huenda pia likaagiza vidonge maalum vya kupunguza uzito. hata hivyo wizara ya ulinzi ya nchi hiyo imesema vidonge hivyo vitatumika kama suluhu ya miwsho kabisa, baada ya mpango wa kupunguza kula, na kufanya mazoezi kushindikana.

Czech ni mwanachama wa NATO na ina wanajeshi wapatao mia saba nchini Afghanistan.

BILA PESA INAWEZEKANA

Mwanamama mmoja nchini Ujerumani amefikisha miaka 15 sasa akiishia maisha yake bila kutumia fedha. Mama huyo mwenye umri wa miaka sitini na tisa aliacha kutumia fedha mwaka 1996.

Image caption Si lazima pesa..

Mwanamama huyo amesema tangu aachane na kutumia fedha kununua na kuuza bidhaa, amekuwa akiishi kwa furaha bila kifani.

Hadithi ya mwanamama huyu ilianza miaka ishirini na mwili iliyopita wakati akiwa mwalimu wa shule ya sekondari. Amesema alipoahamishwa kutoka jiji la Dortmund kwenda eneo la Ruhr, alikutana na jambo ambalo lilibadilisha maisha yake.

Amesema kitu cha kwanza alichokiona ilikuwa idadi kubwa ya watu wanaoishi mitaani bila makazi. Amesema hali hiyo ilimshtua sana kiasi kwamba akaamua kuchukua hatua.

Amesema aliamini kuwa watu masikini wasio na makazi hawahitaji na huwa hawatumii fedha ili kukubalika katika jamii, bali kinachohitajika ni nafasi ya kuwezeshwa.

Amesema baada ya hapo, alifungua duka la kubadilishana bidhaa, liitwalo Gib und Nimm, ikiwa na maana ya Toa na Chukua. Unatoa bidhaa, unaewa bidhaa.

Na kwa taarifa yako

...Wanaume wana damu nyingi mwilini kuliko wanawake. Wanawake wana takriban lita nne na nusu, wakati wanaume wana lita tano na nusu.

Tukutane wiki ijayo.... panapo majaaliwa...