ANC yatupilia mbali hoja za Malema

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Watu wanaomuunga mkono Julius Malema wakimsikiliza nje ya Makao Makuu ANC

Uongozi wa ANC nchini Afrika Kusini umekataa ombi la kiongozi wa Vijana mwenye utata Julius Malema kutupilia mbali kesi yake kuhusu utovu wa nidhamu.

Bw Malema mwenye umri wa miaka 30, anatuhumiwa kwa kusababisha mgawanyiko ndani ya chama na kuleta aibu baada ya kutaka serikali ya Botswana ipinduliwe.

Awali akiwa mshirika wa karibu wa Rais Zuma, Bw Malema amekuwa mkosoaji wake mkubwa.

Kesi ya Bw Malema inaonekana kuwa kipimo cha uongozi wa Bw Zuma katika chama.

Maelfu ya wafuasi wake walipambana na polisi wakati shauri lake lilipoanza kusikilizwa Jumanne. Baadhi walichoma fulana zenye picha ya Bw Zuma.

Mawakili wa Bw Malema wamewasilisha hoja 22 wakitaka kesi hiyo itupiliwe mbali, wanasema amekuwa muathiriwa wa siasa za kumtafuta mchawi na mashtaka yake ni kinyume na katiba.

Hoja zote zilikataliwa na kesi yake itaanza kusikilizwa tena Jumatatu Septemba 5.

Akikutwa na hatia, anaweza kufukuzwa kwenye chama kwani amekuwa katika kipindi cha majaribio kujirekebisha baada ya kumkosoa Bw Zuma mwaka jana. Viongozi wengine wa vijana watano wanakabiliwa na mashataka kama ya Malema.