Uingereza na Marekani zatakiwa kuomba radhi

Abdel Hakim Belhaj Haki miliki ya picha none
Image caption Abdel Hakim Belhaj mkuu wa vikosi vya Libya vinavyompinga Gaddafi

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameroon amesema madai kuwa idara ya ujasusi ya Uingereza MI6 ilihusika katika kuwahamisha washukiwa wa ugaidi wa Libya yanapaswa yachunguzwe na tume maalum ya kujitegemea.

Hii inafuatia nyaraka zilizoonyesha uhusiano wa karibu kati ya idara ya MI6,idara ya ujasusi ya CIA na utawala wa Gaddafi zilizopatikana mjini Tripoli.

Kiongozi wa wapiganaji wanaompinga kanali Gaddafi anasema anazitaka Uingereza na Marekani zimuombe radhi kwa kufanya mipango ya kumpeleka nchini Libya mwaka 2004.

Tume ya uchunguzi ambao bado unaendelea kuhusu madai kuwa idara za masuala ya usalama za Uingereza zilihusika katika unyanyasaji imesema ifanya uchunguzi wake.

Abdel Hakim Belhaj, wakati huo akiwa mtuhumiwa wa ugaidi ambaye sasa ni mkuu wa vikosi vya nchini humo anasema aliteswa baada ya kukamatwa Bangkok.

Anasema alirejeshwa Libya na idara za ujasusi za CIA na MI6 na hatimae kupelekwa gerezani, madai yanayodaiwa kuthibitishwa na nyaraka zilizotumiwa utawala wa Gaddafi.

Kwa mujibu wa Guardian, nyaraka hizi ziligunduliwa na wafanyakazi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika afisi moja iliyokuwa imeachwa wazi mjini Tripoli.

Bw Belhaj amesema kuwa idara za MI6 na CIA hazikushuhudia mateso aliyopata akiwa chini ya ulinzi wa utawala wa awali wa Libya lakini zilimhoji baadae.

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza amesema kuwa tume iliyopo sasa ya uchunguzi kuhusu washukiwa waliozuiliwa iko katika nafasi nzuri ya kufanya uchunguzi kuhusu madai haya mapya.

Taarifa kutoka tume hiyo itakayosimamiwa na Sir Peter Gibson, imesema kama sehemu ya jukumu lake katika kuangalia serikali ilihusika kwa kiasi gani katika utesaji wa waliokuwa wanazuiliwa, itaweza bila shaka kuangalia madai haya mapya ya Uingereza kuhusika katika kuwahamisha washukiwa. Sir Mark Allen, aliyekuwa mkurugenzi wa kitengo cha kukabiliana na ugaidi cha MI6, anasemekana ndiye aliyeandika barua kwa Moussa Koussa, akimshukuru kwa zawadi ya tende na machungwa matamu.Barua hiyo ilipatikana kati ya nyaraka zengine zilizogunduliwa.