Bin Hammam atuhumu ubaguzi Fifa

Aliyekuwa makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka duniani - Fifa- Mohammed Bin Hammam, amelituhumu Shirikisho hilo kwa ubaguzi wa Rangi. Raia huyo wa Qatar amesema kamwe asingekutwa na hatia ya ufisadi iwapo angekuwa mzungu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mohammed bin Hammam

Mohammed Bin Hammam ambaye aliwahi kuwa mmoja wa watu wenye nguvu katika utawala wa soka duniani, ametoa tuhuma hizo kwa watu wanaohusika na adhabu yake ya kufungiwa maisha katika soka.

Katika wavuti wake, Bin Hammam amechapisha barua ambayo ameituma kwa mwenyekiti wa tume ya maadili ya Fifa, Petras Damaseb, ambaye mapema mwaka huu aliwasilisha hukumu yake.

Alikutwa na hatia ya kuandaa mabunda ya fedha kwa ajili ya wapiga kura kutoka Carribean, muda mfupi kabla ya uchaguzi wa urais wa Fifa. Alikuwa akitaka kuchukua nafasi ya Sepp Blatter, lakini baadaye akajiondoa siku chache kabla ya upigaji kura.

Bw Bin Hammam ameandika katika barua hiyo kuwa kama angekuwa ni mzungu, si Blatter wala katibu mkuu wa Fifa Jarome Valke angethubutu kumyooshea kidole.