Wanariadha wa Ugiriki hawana hatia

Mahakama ya rufaa ya mjini Athens imewachilia huru wanariadha wawili wa mbio fupi wa Ugiriki Costas Kenteris na Katerina Thanou kutokana na tuhuma za kughushi kwamba walipata ajali ya pikipiki mwaka 2004.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Costas Kenteris na Katerina Thanou

Jopo la majaji watatu lilitoa uamuzi wa kutokuwepo ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani wanariadha hao wawili kwamba walipanga ajali ili kuepuka kufanyiwa vipimo vya kutumia dawa za kuongeza nguvu katika mkesha wa michezo ya Olympiki ya Athens.

Wanariadha hao mwezi wa Mei walipatikana na hatia ya kusema uongo.

Adhabu ya kufungiwa miezi 33 dhidi ya kocha Christos Tzekos kwa kumiliki dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku, imepunguzwa.

Wanariadha hao ambao kwa sasa wamestaafu mwezi Mei waliapa watakata rufaa dhidi ya adhabu ya kuwasimamisha waliyopewa wakati walipopatikana na hatia ya kusema uongo ilipokamilika kesi yao iliyochukua muda mrefu.

Siku ya Jumatatu, mwendesha mashtaka alipendekeza wanariadha hao wawili waachiliwe na siku ya Jumanne iliposikilizwa kesi yao, majaji walisema hawawezi kusema kama kweli ajali iliyotokea ilikuwa ni ya kupangwa na wanaamini ilitokea kweli.

Majaji hao pia waliwaachia huru madaktari saba waliowatibia wanariadha hao pamoja na watu wawili waliosema walishuhudia ajali hiyo.

Bw Kenteris, mwenye umri wa miaka 37, alishinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 200 katika michezo ya Olimpiki ya Sydney mwaka 2000. Na katika michezo hiyo hiyo Bi Thanou, mwenye umri wa miaka 36, alishinda medali ya fedha katika mbio za mita 100.

Wanariadha hao walilazimishwa kujitoa katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2004 baada ya kushindwa kujitokeza kufanyiwa vipimo vya dawa za kuongeza nguvu, lakini kila mara wamekuwa wakikanusha kufanya lolote baya.