Somalia yakanusha ina magereza ya siri

CIA Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Idara ya ujasusi ya Marekani-CIA

Somalia imekanusha taarifa kuwa Marekani ina kituo cha kuwazuilia watu nchini humo ambako idara ya ujasusi ya Marekani inasaidia kuwahoji washukiwa wa ugaidi katika mji mkuu wa Mogadishu.

Makundi ya kutetea haki za bindamu ya Uingereza yanasema yanaushahidi kuwa kituo hicho kipo chini ya ardhi katika makazi ya Rais na kuwa baadhi ya wanaozuiliwa kati yao kuna walio na umri wa miaka 14.

Kundi hilo linasema mtu mmoja alikamatwa kutoka Kenya na kuzuiliwa miezi 18 bila ya kumuona wakili ama kutoka nje.

Maafisa wa Marekani bado hawajasema chochote hadi sasa.

Waziri Mkuu wa Somalia Abdiweli Mohammed Ali akizungumza na BBC amekanusha ripoti hizo kuhusu kuwepo kituo cha kuwazuilia watu.

Hatavivyo, amekiri kuwa Marekani inaisaidia serikali yake kuimarisha masuala ya usalama nchini humo.

Wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabab wanaofahamika kuwa na uhusiano na al-Qaeda wanadhibiti eneo kubwa la kusini na kati mwa Somalia.

Serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ipo mjini Mogadishu ambapo inaendesha shughuli zake zote kutoka hapo.

Mwezi July, jarida moja la Marekani lilizungumzia kuwepo kituo cha kuwazuilia watu nchini Somalia.

Marekani imefanya mashambulio kadhaa ya angani dhidi ya al-Shabab nchini Somalia katika miaka ya hivi karibuni. Kuna kituo cha kijeshi cha Marekani katika nchi jirani ya Djibouti.