Misri katika hali ya tahadhari

Misri imetangaza hali ya tahadhari kufuatia maandamano katika mitaa ya Cairo, baada ya kushambulia ubalozi wa Israel siku ya Ijumaa usiku.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waandamanaji wakishambulia ubalozi wa Israel

Majeshi ya usalama yalirusha mabomu ya kutoa machozi na magari maalum ya kutuliza ghasia kutawanya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe na mabomu ya petroli. watu watatu wamekufa, wamesema maafisa.

Waandamanaji waliingia katika jengo la ubalozi na kurusha nje nyaraka mbalimbali, wamesema maafisa.

Israel imewarejesha nyumbani balozi wake na maafisa karibu wote.

baraza la kijeshi linalotawala Misri linakutana siku ya Jumamosi kujadili hali ilivyo.

watu watatu walikufa, imesema wizara ya afya, mmojawapo kwa mshituko wa moyo. Zaidi ya watu 1,000 wamejeruhiwa.

Mamia ya waandamanaji walisalia karibu na ubalozi wa Israel hadi majira ya asubuhi, wakichoma moto matairi mitaani na kuimba nyimbo dhidi ya ya watawala wa kijeshi wa Misri.

Polisi wa kituliza ghasia walikuwepo mitaani na milio ya risasi ilisikika, anasema mwandishi wa BBC Bethany Bell mjini Cairo, huku hewa ikiwa imejaa moshi wa mabomu ya machozi.

Wafanyakazi sita wa ubalozi walikwama ndani ya jengo wakati wa ghasia hizo na kulazimika kuokolewa na makomando wa Misri, afisa mmoja wa Israel ameiambia BBC.

Afisa huyo ameishukuru Misri kwa kuwaachilia wafanyakazi wa Israel na kuelezea ghasia hizo kama "pigo kubwa katika pazia la amani" kati ya nchi hizo mbili.

Tukio hilo lilikuwa "ukiukwaji mbaya" wa diplomasia ya kawaida, amesema afisa huyo.

Misri ni moja ya nchi pekee mbili za Kiarabu ambazo zimeweka moango wa amani na Israel. Nchi nyingine ni Jordan.

Hali ya kupinga Israel imekuwa ikiongezeka nchini Misri, ikichochewa na vifo vya watu polisi watano wa Misri mwezi Agosti waliokuwa katika mpaka wa Israel.

Shirika la habari la serikali la Misri Mena limesema watu 448 walijeruhiwa katika mapigano usiku wa kuamkia Jumamosi.

Vurumai hizo zilianza baada ya sala ya Ijumaa, wakati maelfu ya watu walikusanyika katika eneo la wazi la Tahrir na kudai mabadiliko ya haraka ya kisiasa, baada ya kuondolewa kwa rais wa zamani Hosni Mubarak mwezi Februari.

Afisa mmoja wa Israel amesema wafanyakazi 80 wa ubalozi, akiwemo balozi mwenyewe na familia zao walisafirishwa kwa ndege usiku kupelekwa Israel.

Ubalozi mdogo wa Israel umesalia mjini Cairo.