Mancini amvua unahodha Carlos Tevez

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amemvua moja kwa moja unahodha timu hiyo Carlos Tevez.

Haki miliki ya picha elvis
Image caption Mancini na Tevez

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina katika heka heka za kuuanza msimu huu alitafuta bila mafanikio kujiunga na klabu mpya na nafasi yake ya unahodha sasa inachukuliwa na mlinzi Vincent Kompany.

Mancini amesema: "Carlos alikuwa anataka kuhama kwa sababu za kifamilia. Naheshimu matakwa yake lakini Carlos bado yupo hapa kwa sababu hatukupata suluhisho.

"Niliamua msimu huu Vinnie Kompany ndiye atakuwa nahodha wetu mpya."

Tevez alicheza mechi moja akiwa mchezaji wa akiba kwa City msimu huu, akichukua nafasi ya Sergio Aguero katika mechi ambayo walishinda kwa mabao 3-2 dhidi ya Bolton tarehe 21 mwezi wa Agosti.

Ametajwa atakuwemo katika kikosi kitakachokabiliana na Wigan siku ya Jumamosi, lakini sasa hatakuwa nahodha wa timu.

Kompany mchezaji wa kimataifa wa Ubelgiji alijiunga na City akitokea timu ya Hamburg mwaka 2008 na amecheza mechi 53 katika mashindano yote msimu uliopita. Ameshawahi kuwemo katika kuwania tuzo mchezaji bora wa mwaka.

Mancini ameongeza kueleza kwamba Tevez bado ataendelea kuwa mchezaji muhimu katika kikosi chake msimu huu, wakati timu hiyo ikijiandaa kwa mechi za Ubingwa wa Ulaya. Amesema: "Ni mchezaji hodari sana kwetu anayeweza kufunga mabao 20 kwa msimu mmoja."

Tevez hivi karibuni alizungumzia kuyumba kwa uhusiano wake na Mancini na pia kuhusishwa kwake na kuihama klabu hiyo.

Kompany ameiongoza Man City katika mechi tatu walizocheza za Ligi Kuu ya England msimu huu - City imeshinda mechi zote hizo wakiwa wanatafuta ubingwa walioukosa tangu mwaka 1968.