Ferguson akemea rafu ya Kevin Davies

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amekemea rafu aliyocheza Kevin Davies wa Bolton iliyomuacha Tom Cleverley kwenye hofu huenda amevunjika mguu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Sir Alex Ferguson

Cleverley alitolewa nje katika kipindi cha kwanza kwenye mechi ambayo Manchester United iliiadhibu Bolton mabao 5-0, baada ya kufanyiwa rafu nzito na nahodha huyo wa Bolton na alitolewa uwanjani akiwa amevalishwa kiatu maalum cha kumkinga.

Kiungo huyo wa Manchester United atafanyiwa uchunguzi wa kina kuona ukubwa wa jeraha lake.

"Huenda atakuwa amevunjika mguu, itakuwa ni bahati mbaya," Ferguson ameiambia BBC. "Tunataraji itakuwa hivyo, ilikuwa rafu mbaya."

Davies hakuonywa kutokana na rafu hiyo lakini muda mfupi baadae akaoneshwa kadi yake ya 100 ya manjano tangu aanze kucheza Ligi Kuu ya Soka ya England baada ya kumchezea vibaya Patrice Evra.

Ferguson amesema atachunguza kikosi chake kabla hawajasafiri kuelekea Ureno kwa ajili ya pambano la Ligi ya Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Benfica siku ya Jumatano.

"Tutaona namna tulivyo siku ya Jumapili," alisema Ferguson. "Jonny Evans ameumia goti, Patrice Evra naye aligongwa gotini."