Mwanawe Gaddafi Saadi 'awasili Niger'

Image caption Gaddaffi's Son Saad

Waziri wa masuala ya haki wa Niger amesema kuwa Saadi Gaddafi alikuwa katika msafara uliokuwa ukielekea mji mkuu wa Niger, Niamey.

Haijulikani Gaddafi mwenyewe yuko wapi kwa sasa. Lakini amesema hataondoka nchini Libya.

Wapiganaji wanaokabiliana na vikosi vya Gaddafi sasa wanadhibiti maeneo mengi nchini Libya, ukiwemo mji mkuu Tripoli. Wamekuwa wakijaribu kuchukua udhibiti wa miji mingine, iliyo chini ya wale wanaomuunga mkono Gaddafi, ikiwemo Bani Walid na Sirte.

Mapambano

Siku ya Jumapili, vikosi vya waasi vilianza mashambulio katika mji wa Bani Walid, vikisaidiwa na mashambulio ya angani ya Nato. Maafisa wanasema vikosi vyao sasa viko karibu kufika katikati mwa mji wa Bani Walid.

Baadhi ya watu wa jamii ya Gaddafi wamekimbilia Algeria. Misafara kadhaa ya watu waliokuwa wakimuunga mkono Gaddafi imeonekana ikivuka mpaka wa kusini mwa Libya na kuingia Niger hivi karibuni.

Msemaji wa serikali ya Niger na waziri wa masuala ya haki Marou Amadou amesema kuwa Saadi Gaddafi alikuwa kwenye msafara huo na watu wengine wanane. Bwana Amadou anasema msafara huo ulikuwa njiani kuelekea Agadez kaskazini mwa Niger na kwamba Saadi pamoja na wale alioandamana nao aliruhusiwa kwa misingi ya kibinaadamu.

Serikali ya Niger imetambua utawala wa baraza la kitaifa la mpito, lakini ikasema bado hawajaamua kama watamruhusu Gaddafi kuingia nchini.